Chama cha Labour chaahidi neema Uingereza – DW – 14.06.2024

Uzinduzi huo wa ilani ya uchaguzi ya chama cha Labour ulikuja siku mbili baada ya chama cha Conservative kuwaahidi wapigakura makato zaidi ya kodi, katika kampeni ambako ufanisi wa mipango ya matumizi ya vyama hivyo vikuu umewekwa chini ya uchunguzi wa karibu.

Licha ya uongozi wa mkubwa wa Labour katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura, Starmer anapambana kushinda madai ya Wafafidhina kwamba chama chake kitatumia pesa za umma bila kujali na kupandisha kodi kwa watu binafsi.

Starmer ameondia suala la kuongeza kodi ya mauzo ya VAT, viwango vya kodi ya mapato na Bima ya taifa, ambayo hulipia huduma za afya za serikali, pensheni na ukosefu wa ajira. Anasema badala yake chama cha Labour kitalenga kukuza ukuaji wa uchumi iwapo kitashinda.

Aliahidi kurejesha utulivu wa kiuchumi baada ya misukosuko ya miaka ya hivi karibuni ambayo ilisababisha mfumuko wa bei kufikia asilimia 11.1 mnamo Oktoba 2022 – kiwango chake cha juu zaidi katika miaka 40.

UK Salford | mdahalo wa TV kati ya Waziri Mkuu Sunak na Kiongozi wa Labour Starmer
Keir Starmer akichuana kwenye mdahalo wa televisheni na Waziri Mkuu Rishi Sunak.Picha: Jonathan Hordle/ITV via Getty Images

Hata hivyo Starmer na waziri wa fedha mtarajiwa Rachel Reeves wanaonekana kuwa na nafasi ndogo ya kufanya ujanja, wakati ukuaji wa uchumi ukisimama mwezi Aprili baada ya kuimarika kutoka kwenye mdororo katika robo ya kwanza.

Mpango wa kuaminika wa muda mrefu

Wachumi wanasema hata hivyo kwamba serikali ijayo inaweza kusaidiwa na kushuka kunakotarajiwa kwa viwango vya riba na mfumuko wa bei kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Starmer alisema katika uzinduzi wa ilani ya chama kaskazini mwa London, kwamba wanao mpango wa kuaminika wa muda mrefu.

Soma pia: Truss ajiuzulu baada ya wiki sita kama waziri mkuu Uingereza

“Kile ambacho ilani hii inawakilisha ni mpango unaoaminika wa muda mrefu, mpango uliojengwa kwa misingi thabiti yenye hatua za kwanza zilizo wazi, sheria kali za matumizi ambazo zitapunguza kodi na mfumuko wa bei,” alisema Starmer mjini Manchester.

“Amri ya usalama wa mipakani kuvunja magenge ya wahalifu, nishati kubwa ya Uingereza kupunguza bili nyumbani kwako, polisi zaidi katika mji wako, kukabiliana na tabia zisizofaa katika kijamii na walimu wapya 6500, kuwapa watoto wako mwanzo wa maisha wanaostahili.”

Kama ilivyokuwa mwaka wa 1997, Tony Blair aliposhinda kwa kishindo baada ya miaka 18 ya utawala wa Tory, Starmer anajua kwamba anahitaji kuwahakikishia wapiga kura waliochanganyikiwa kwamba Lacour inaweza kuhakikisha utulivu na uwezo wa kiuchumi.

Mtetezi wa biashara, wafanyakazi

Katika uchaguzi uliopita wa 2019, mtangulizi wake Jeremy Corbyn alisimamia sera kali zilizojumlisha mapendekezo ya urekebishaji upya wa viwanda muhimu, na nyongeza ya kodi kwa watu wenye kipato cha juu.

Uingereza| Wahamiaji wakiwa kwenye mashua
Chama cha Labour kimeahidi kufutilia mbali mpango wa chama cha Conservative kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi ambao maombi yao yalikataliwa.Picha: Jordan Pettitt/PA Wire/empics/picture alliance

Starmer alichukuwa uongozi baada ya chama cha Labour kushindwa vibaya na Wahafidhina wakioogonzwa na Boris Johnson, Amekirejesha chama kwenye mrengo wa kati usiotisha, na kuahidi kwamba kinasimamia biashara pamoja na wafanyakazi.

Sunak alidai kuwa Ilani ya Labour ilithibitisha kuwa chama hicho cha upinzani kitaleta kodi kubwa zaidi katika historia, ingawa mzigo wa jumla wa kodi umeongezeka na kurekodi viwango vya juu chini ya uangalizi wake.

Soma pia:Labour yashinda viti vya ubunge katika ngome ya Conservative Uingereza 

Waingereza wamevumilia kipindi ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha msukosuko wa kisiasa, na mawaziri wakuu watano wa Conservative tangu 2010, na watatu katika kipindi cha miezi minne tu ya mwaka 2022.

Hayo yalikuwa kwa sehemu kubwa matokeo ya mchakato wa Brexit, uliopelekea taifa hilo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.

Baadi ya maafisa waandamizi wa Conservative wameanza kimsingi kukubali kushindwa, wakiwahimiza wapigakura kuzuwia ukubwa wa wingi wa Labour.

Moja ya majukumu ya kwanza ya Starmer ikiwa atajikuta katika mtaa wa Dawning Julai 5, itakuwa kujindaa kwa mkutano wa kilele wa NATO wiki inayofuata na kuandaa mkutano wa viongozi wa Ulaya.

Anasema atafutilia mbali mpango wa chama cha Conservative wa kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi ambao maombi yao yalikataliwa na atatambua uhuru wa Palestina kama sehemu ya mchakato wa amani.

Chanzo: Mashirika

Related Posts