DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC, kimefikia makubaliano na chama cha mrengo wa kati cha Democratic Alliance (DA) pamoja na  chama cha Kizulu cha Inkatha Freedom Party (IFP), kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hatua hiyo imefikiwa baada ya ANC kuambulia asilimia 40.18 pekee ya kura na kupata viti 159 vya wabunge kati ya 400 vya Bunge la Taifa katika uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Mei mwaka huu.

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kinachoongozwa na John Steenhuisen, kilipata 21.18 % ya kura huku chama Inkatha Freedom Party (IFP) kilichoungana ANC kwenye muungano huo, kikipata asilimia nne ya kura na wabunge 17.

John Steenhuisen na Rais Cyril Ramaphosa

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Kiongozi wa chama cha DA, John Steenhuisen mbali na kuthibitisha makubaliano, amesisitiza sura mpya katika historia yao imefikiwa.

Aidha, amesema DA kitamuunga mkono Ramaphosa kama rais wa Taifa hilo kwa awamu nyingine na kusisitiza kuendeleza siasa mpya za ushirikiano.

Ameongeza kuwa makubaliano hayo yalifikiwa baada ya “mazungumzo makali lakini yaliyokomaa” na kwamba yanaakisi sehemu nyingi za ilani ya DA.

Pia amesema makubaliano hayo ni halisia katika uhitaji wa mifumo ambayo bila shaka itatokea kwenye serikali ya vyama vingi.

“Watu pia wametuambia kwamba wakati wa siasa mpya ya ushirikiano na utatuzi wa matatizo umefika.

“Kuanzia leo DA itatawala kwa pamoja Jamhuri ya Afrika Kusini kwa moyo wa umoja na ushirikiano… tunafanya hivyo kwa ajili ya mamilioni waliopiga kura kwa ajili yetu na Waafrika Kusini wote wanaotamani serikali bora”, amesema.

Related Posts