Dortmund yamtema kocha Terzic | Mwanaspoti

DORTMUND, UJERUMANI: BORUSSIA Dortmund imetangaza kuachana na kocha Edin Terzic baada ya pande mbili kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba.

Jambo hilo limetokea ikiwa umepita muda usiozidi wiki mbili tangu Dortmund ilipocheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuchapwa mabao 2-0 na Real Madrid kwenye kipute kilichofanyika Wembley.

Hata hivyo, pande hizo mbili zimefikia makubaliano ya kila mmoja achukue virago vyake bvaada ya mazungumzo ya siku kadhaa. Katika taarifa iliyotolewa na tovuti ya klabu ya Dortmund ni kwamba Terzic alikuwa na mipango ya kwenda kukabiliana na changamoto mpya baada ya miaka tisa ya kuwapo kwenye kikosi hicho cha Westfalenstadion.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 41 aliwaambia mashabiki wa Dortmundu: “Wapendwa mashabiki wa Borussia, inaniumiza sana kuwaambia kwamba naachana na BVB. Ilikuwa heshima kubwa kuingoza klabu kwenye ubingwa Kombe la DFB na hivi karibuni kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Naitakiwa Borussia Dortmund kila la heri, asanteni na kwaherini.”

Mkurugenzi wa michezo wa Dortmund, Sebastien Kehl alisema: “Edin ni shabiki wa Borussia nje ndani ni mtu safi na aliyejitolea kwa asilimia 100 hapa BVB. Tumepata uzoefu wa mengi pamoja. Kilikuwa kitu kizuri kufanya kazi na Edin.”

Dortmund ilimaliza kwenye nafasi ya tano huko kwenye Bundesliga msimu uliopita, kitu ambacho hakikuwa kizuri kwa kocha Terzic, ambaye msimu mmoja kabla alikaribia kuipa taji la ligi hiyo miamba hiyo. Dortmund ilikaribia kabisa kunyakua taji la Bundesliga katika msimu wa 2022-23 kabla ya kutoa sare dhidi ya Mainz 05 kwenye mechi ya mwisho na hivyo kuwapa nafasi Bayern Munich kubeba ubingwa kwa tofauti ya mabao.

Related Posts