Gharama kikwazo matibabu kwa wenye tatizo la afya ya akili

Dar es Salaam. Gharama za matibabu na unyanyapaa ni baadhi ya vikwazo vinavyotajwa kutatiza watu wenye changamoto ya afya ya akili kupata huduma za afya.

Imeelezwa kuwa  wagonjwa hushindwa kugharimia huduma kutokana na ugumu wa maisha jambo linalochangia ndugu kuwatekeleza wodini kwa muda mrefu.

Changamoto hizo zimeelezwa na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Akili Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dk Praxeda Swai leo Ijumaa Juni 14, 2024 wakati akizungumza na Uongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) iliyofika kwenye Idara hiyo kutoa msaada wa mavazi kwa wagonjwa wenye  changamoto ya afya ya akili.

Msaada huo kwa wagonjwa wenye changamoto ya afya ya akili, ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Baba Duniani ambayo hufanyika Juni 16 ya kila mwaka.

Akipokea msaada huo, Dk Praxeda ametaja changamoto wanayokumbana nayo ni baadhi ya wagonjwa wao kushindwa kumudu bili za matibabu.

“Wanashindwa kumudu gharama za matibabu kutokana na changamoto za kiuchumi, unakuta  wengine wanashindwa kuwa na bima ya afya hivyo hulazimika kuchangia huduma hivyo inakuwa shida kwao,”amesema.

Baadhi ya wagonjwa wengine wakishatibiwa, Dk Praxeda amesema wanabaki kwa muda mrefu wodini kutokana na ndugu kutojitokeza kuwachukua.

Mtaalamu huyo wa magonjwa ya akili, amesema kama jamii itaachana na unyanyapaa, wagonjwa wenye changamoto ya afya ya akili hupata maendeleo ya haraka punde wanapopatiwa matibabu.

KIlio cha gharama kilipazwa pia na mmoja wa wagonjwa wodini hapo akiiomba Serikali huduma hizo zitolewe bure.

“Serikali iangalie namna ya kutusaidia, tupate matibabu, tunashindwa kumudu gharama za dawa,”amesema  mmoja wa wagonjwa.

Katika hatua nyingine akizungumzia warahibu wa dawa za kulevya, Dk Praxeda amesema kwa siku wanaofika kliniki kupata dawa ni kati ya warahibu 800 hadi 900 na wengine hupatiwa msaada wa kisaikolojia.

Wataalamu wa masuala ya saikolojia wanaeleza kuwa, changamoto ya akili ni janga duniani na katika kila sekunde 40 watu watatu wanapoteza maisha kutokana na tatizo hilo.

Wanaeleza kuwa dalili ya changamoto ya afya ya akili ni kukosa usingizi vizuri kunakosababisha wengine kuchukua hatua za kunywa kilevi, kukosa hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake na wanaume.

Pia, kuongezeka uzito ghafla wakati vyakula havijabadilika, hasira   za mara kwa mara, magonjwa ya vidonda vya tumboni, ngozi ini na moyo.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Victor Mushi amesema katika kusherekea Siku ya Baba Duniani, wameona ni vyema kutafuta namna ya kuinua hali ya watu wanaoishi na changamoto ya afya ya akili.

“Tumeamua kufanya hivi kuelekea siku ya kinababa kwa sababu ukiangalia takwimu kina baba hatutoi nafasi ya kuzungumza matatizo ya akili tunayokabiliana nayo.

“Wapo wanaume wengi wanapambana na hali mbalimbali ya shida ya akili na matokeo yake takwimu zinaonyesha kwa kila wanaume 100,000 wanaojiua ni 12 kila mwaka,”amesema Mushi.

Hali hiyo ni tofauti na wanawake, Mushi amesema kila wanawake 100,000 duniani watano pekee ndio wanaojiua.

Mushi amesisitiza kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Mwananchi kama sehemu ya jamii inataka kubadili  mfumo wa maisha wa wanaume, wawe huru kueleza  magumu wanayopitia na kutafuta msaada wa haraka wanapopata changamoto.

Inakadiriwa watu milioni saba wanaishi na matatizo ya akili na utumiaji wa dawa za kulevya na zaidi ya milioni 1.5 wameathiriwa na matatizo ya unyogovu pekee, huku idadi kubwa ya walioathiriwa na matatizo ya unyogovu ni wanawake.

Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zinaonyesha kuna ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili kwa asilimia 17 kwa mwaka 2020/21 huku wanaume wakikabiliwa zaidi na tatizo hilo ikilinganishwa na wanawake.

Kati ya wagonjwa wa nje 24,014 walioonwa kwa kipindi hicho, wanaume walikuwa 15,205 ikilinganishwa na wanawake 8,809.

Kuhusu bajeti, Serikali imetenga Sh9.3 bilioni kwa ajili ya huduma za afya ya akili nchini kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Related Posts