Italia inataka mataifa ya G7 yawekeze zaidi Afrika. – DW – 14.06.2024

Viongozi wa kundi la nchi tajiri kiviwanda duniani,G7, wanaendelea na mkutano wao kwa siku ya pili leo, utakaojikita kwenye suala la Uhamiaji.

Katika ajenda hiyo watajielekeza zaidi kutafuta njia za kukabiliana na biashara ya usafirishaji watu pamoja na kuongeza uwekezaji katika mataifa wanakotokea wahamiaji.

Italien G7-Gipfel in Puglia
Picha: Yara Nardi/REUTERS

Jana katika ufunguzi wa mkutano huo waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni alisisitiza juu ya umuhimu wa viongozi wenzake wa G7 kulipa umuhimu suala hili la wahamiaji na hususan kwa kulisaidia bara la Afrika. Na leo Ijumaa mkutano huo utalijadili kwa mapana bara la Afrika na Uhamiaji.

Uhamiaji ni suala linalopewa umuhimu na Italia yenyewe kama nchi pamoja na waziri mkuu wake Giorgia Meloni ambaye anataka uwekezaji uongezwe barani Afrika na mataifa ya bara hilo yapate ufadhili kama njia ya kupunguza shinikizo linalowafanya wakaazi wa bara hilo kukimbilia nchi za Ulaya.

Jana viongozi walitowa ahadi za kuipatia msaada wa  mabilioni ya dola Ukraine.

Rais Volodymyr Zelensky akishiriki mkutano wa G7,Italia
Mkutano wa G7- Borgo EgnaziaPicha: Nicholas Berardo

Rais Volodymyr Zelensky aliyeshiriki mkutano huo alisaini makubaliano ya kiusalama na Marekani lakini pia na nchi nyingine za kundi hilo la G7 linalozijumuisha,Marekani,Uingereza,Ujerumani,Italia,Japan,Canada na Ufaransa.

“Tumeshasaini mikataba saba kuhusu usalama na mataifa yote ya G7. Kwa ujumla tumesaini mikataba 17 na tunajiandaa kusaini mingine 10.

Rais Joe Biden aliyefanya mkutano wa pembeni na Zelensky alisema mkataba wa kiusalama uliosainiwa baina ya Marekani na Ukraine unapaswa kutuma Ujumbe kwa Urusi kwamba haiwezi kuigawa Ukraine na washirika wake.

Kwa upande mwingine Japan ilisaini na Ukraine mkataba wa miaka 10 wa kiusalama,ulinzi na msaada wa kibinadamu,kama alivyofafanuwa waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida.

“Japan itashirikiana na mataifa mengine ya G7 na yale yenye mitazamo sawa na yetu kutowa msaada mkubwa kwa Ukraine.”

Pamoja na yote viongozi wa G7 walionesha kuwa na mgawanyiko kuhusiana na kifungu kilichowekwa katika azimio la mwisho la mkutano huo kinachohusiana na haki ya utoaji mimba.

Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: Vatican Media/Catholic Press/picture alliance

Italia imemtaka waziri mkuu wake Giorgia Meloni asikubali kuunga mkono ajenda hiyo. Mgongano huo umejitokeza wakati ambapo kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani  Papa Francis amepangiwa kuhutubia mkutano huo wa Puglia leo Ijumaa.

Atakutana pia na viongozi kadhaa pembezoni mwa mkutano huo akiwemo rais Zelensky vile vile rais wa Kenya William Ruto,waziri mkuu wa India  Narendra Modi,na Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki miongoni mwa wengine.

 

Related Posts