Kama una kundi hili la damu fahamu changamoto zake, namna ya kuzitatua

Dar es Salaam. Makundi adimu ya damu ni yale yenye vinasaba (-) ambayo yana uwezo wa kuyachangia makundi yote, mfano kundi la damu la O – (O negative, yaani hasi).

Kuna makundi makuu manne ya damu ambayo ni A, B, AB, O na kila kundi lina aina yake ya vinasaba ambavyo ni (+) na (-).

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Damu leo Juni 14, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji wa Damu Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Kizito Tambe anasema licha ya kukusanya damu nyingi, bado wanakabiliwa na uhaba kwa kundi la wenye vinasaba hasi.

Hatua hiyo inafanya makundi hayo yaendelee kuwa adimu kupatikana nchini na hivyo kusababisha uhaba wa wachangiaji damu na changamoto ni namna ya kuwapata watu hao kwa ajili ya kuchangia damu.

Anasema asilimia moja ya Watanzania wana kundi maalumu liitwalo ‘negative’, huku asilimia 99 yao wakisalia kuwa kundi ‘positive’.

“Hili kundi la negative A- B- AB- 0- kwa ujumla wake wana shida na kwenye hospitali nyingi damu zao hazipo, wao hawapokei damu nyingine, vinginevyo zaidi atapokea wa kundi lake au mwenye kundi O – ambaye anaweza kumpa yeyote mwenye negative ila yeye hapokei nyingi zaidi ya O- mwenzake,” anafafanua Kizito.

“Wenye damu za vinasaba positive ni wengi, damu zao zipo tu, mara nyingi haisumbui sana, ila wale wa hasi ni wachache, ni asilimia moja tu ya Watanzania unaweza kukuta hata hapa Dar es Salaam wapo 100, sasa hawa kuwapata ni vigumu sana na ili kuwe na ahueni lazima wawe na utamaduni wa kuchangia damu.”

Kizito anasema wamelazimika kutengeneza vikundi vya mitandao ya kijamii (WhatsApp) kwa ajili ya mawasiliano, ikitokea mgonjwa anatakiwa kuongezewa damu kundi husika wanajulishwa wenzake ili waweze kumchangia damu hiyo.

“Makundi haya yana watu 300 wenye kundi maalumu wa damu hiyo, ikitokea mtu anatakiwa kuongezwa damu wanasaidiana ili kuhakikisha mwenzao anapata damu kwa wakati,” anasema Tambe.

Anasema changamoto iliyopo kwa watu wenye makundi ya damu hiyo wapo wachache, kundi ambalo linaongoza kuwa chini ya asilimia moja ni AB negative ambayo ipo asilimia moja.

Ikifuatiwa na watu wenye kundi la damu B ni asilimia 1.3, A wapo asilimia 1.5 na O wapo asilimia 1.7.

Kutokana na uchache wa makundi ya damu hizo, wananchi wametakiwa kwenda kupima damu ili kujua wapo kwenye kundi lipi, itasaidia kufahamiana pindi wanapotaka kuoana.

“Utakuta mimba nyingi zinaharibika, mtu anaenda kwa mganga kumbe ni kundi la damu alilokuwa nalo la hasi, kila akishika mimba zinatoka au watoto wanakufa na ukishakuwa na damu tofauti na mume wako watoto wanakufa, baadaye mnatafuta chanzo ni nini, kumbe ni wewe mwenyewe,” anasema Kizito.

Anasema wanawake waliofika umri wa kuzaa wanatakiwa watambue damu zao zipo kwenye kundi gani na hata wanapokutana na mwanamume mwenye kundi la damu hasi watapewa ushauri nini kifanyike

Anatolea mfano mwanamume akiwa na kundi la damu hasi na mwanamke akiwa chanya akapata mimba mtoto atakufa, kwa sababu mwili wa mwanamke utagundua kuna kitu katika mwili wake siyo cha kawaida.

“Mwili wa mwanamke utakachofanya utatengeneza kinga bila kujua zitamuathiri au kumuua mtoto aliye tumboni, matokeo yake baada ya miezi mitatu mimba inaharibika,” anasema.

Kizito anasema inapogundulika wanandoa au wapenzi hao damu zao mmoja yupo kwenye kundi hasi na mwingine chanya, mama anatakiwa kuchoma sindano kwa ajili ya kurudisha kinga ili kuzuia mimba isiharibike.

“Ikitokea mwanamke mwenye kundi la damu hasi akimpata mwanaume mwenye kundi hilo hawatakuwa na shida, mtoto atazaliwa bila matatizo na vilevile wote wawili wakiwa positive ambao wapo zaidi ya asilimia 98 watatengeneza kitu kinachofanana mtoto atazaliwa,” anasema.

Kizito anaelezea kuwa katika benki ya damu kundi la hasi huwa hawatunzi kwa kuwa damu inakaa siku 35, unaweza ukaiweka asitokee mhitaji, na ikitokea wameenda shule mbalimbali au kwenye taasisi wanaweza wakampata mmoja mwenye kundi hilo.

Anasema ikitokea wamepata damu ya kundi hilo, wanalazimika kuitolea taarifa haraka kama kuna mgonjwa anahitaji ipelekwe ili isije kuharibika.

Alitolea mfano kuna mgonjwa anatakiwa kuongezewa damu hiyo kwenye benki ya damu hawana, hulazimika kutumia gharama kubwa ili kuitafuta, ikiwemo kwa watu wanaojulikana na kwenye makundi ya kijamii ya Whatsapp.

“Watu wakichangia damu inakaa siku 35 kisha inaharibika, lakini ukiitenganisha ukiondoa maji ikabakia chembe nyekundu zina uwezo wa kukaa hadi siku zaidi ya 45 na nyingine zinakaa hadi mwaka, inategemea na vifaa bora vya kuhifadhia na umeme usiokatika,” anasema.

Anasema sasa hivi wanatengeneza mazao ya damu kuliko damu yenyewe, kwani uwezo wa kutunza ni mdogo, hivyo ukitenganisha thamani inaongezeka.

Kizito anasema siyo kila ugonjwa unahitaji damu yote, kuna magonjwa mengine yanahitaji chembe nyekundu, huku wagonjwa wengine wakihitaji maji au chembe sahani tu, vingine anakuwa navyo.

“Ukimpata mgonjwa mwenye malaria, anawekewa chembe nyekundu tu, maji anakuwa nayo na mwenye ugonjwa wa selimundu au saratani anahitaji kuwekewa chembe sahani, huku chembe nyingine akiwa anazo.

“Damu ukiitenganisha unaipa thamani kwa kuwa utawapa watu zaidi ya watatu, lakini ukitoa damu na kumpa mtu mwingine unaipunguzia thamani, utakuta mgonjwa hahitaji yote, matokeo yake inamletea madhara,” anasema Kizito.

Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Lulu Chirande anasema changamoto ni damu chache, lakini kuna aina ya makundi yenye uhitaji zaidi.

“Tunawahitaji zaidi wenye makundi O wachangie kwa wingi, kwa maana hii inahitajika zaidi na wanapewa wengi zaidi ikilinganishwa na makundi mengine. Tunawahamasisha wenye makundi haya kuchangia kwa wingi zaidi kwa kuwa kundi hili linamchangia yeyote, lakini halipokei damu yoyote,” alisema Dk Lulu, ambaye pia ni Daktari bobezi wa magonjwa ya damu na saratani za watoto.

Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wa Hospitali ya Taifa ya Muhumbili, Stella Rwezaura anasema watu wenye damu makundi hasi ya O, A, B na AB wanatoka nje ya nchi ambao ni wazungu na Wahindi, kwa upande wa Afrika wenye makundi hayo ni wachache sana.

Dk Rwezaura anasema benki za damu zinawasiliana na watu wenye makundi hayo, huwa wanapigiwa simu wanapohitajika kumtolea mgonjwa damu.

Anasema katika benki ya damu, wanatunza chupa mbili hadi tano kama za makundi ya damu hizo, ikitokea wagonjwa ni wengi wanaitwa watu ambao wanajulikana hospitalini hapo kwa ajili ya kuchangia.

Dk Rwezaura anasema changamoto iliyopo damu hizo hazipatikani kwa wingi, inatokea mgonjwa anatakiwa kuongezewa lakini wanaochangia walishatoa kwa wengine, hivyo inalazimika kusubiri, hali inayochangia wengine kufariki dunia.

Related Posts