MASHINDANO yaliyoboreshwa na kuongezwa ukubwa ya Klabu Bingwa ya Dunia yaliyopangwa kufanyika Marekani mwakani, yameingia dosari baada ya klabu na ligi kuyapinga na kutishia kwenda mahakamani kwa hoja kuwa yanaongeza idadi ya mechi zinazovuruga ligi za nchi wanachama na pia kuweka rehani afya za wachezaji.
Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) limeboresha mfumo na ukubwa wa mashindano hayo kutoka kushirikisha mabingwa wa soka wa mabara hadi kufikia timu 32, hali inayolazimisha mashindano hayo kuchezwa kwa siku 29, kuanzia Juni 15 hadi Julai 13 mwaka 2025, kipindi ambacho nchi zinakuwa katika mapumziko ya shughuli za soka.
Msimu ya soka katika nchi nyingi huanza kati ya Julai mwishoni na Agosti mwanzoni na kumalizika Mei mwaka unaofuata, hivyo katika kipindi hicho wachezaji huenda mapumziko isipokuwa wale ambao timu zao za taifa zinakuwa kwenye mashindano ya kimataifa. Wachezaji hao wanapomaliza majukumu yao kwa mataifa yao, hupewa mapumziko zaidi klabuni ili kupumzisha miili yao kabla ya msimu mpya.
Kwa hiyo, ikiwa mashindano hayo ya klabu yatachezwa katika kipindi hicho, maana yake ni kwamba klabu nzima itakuwa haijapata mapumziko na hivyo kuhitaji muda zaidi kabla ya kurudi kwenye ligi ya nchi yake, hali ambayo itakuwa ni vurugu zaidi kwa vyama vya soka vya nchi.
Wachezaji watakaohusika katika mashindano hayo ya Fifa wanaweza wasipate mapumziko makubwa kwa sababu kabla ya mashindano hayo wanaweza kuwa wanawakilisha nchi zao katika mashindano mengine ya mabara yao.
Mfano, fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2024 zinafanyika kuanzia Juni 14 na kumalizika Julai 11. Wachezaji watakaokuwa nan chi zao nchini Ujerumani kwenye fainali hizo, wanaweza kuwa ndio wanatakiwa na klabu zao kushiriki Klabu Bingwa ya Dunia mwakani nchini Marekani. Yaani kipindi cha mapumziko cha mwaka huu watakuwa Euro 2024 na kipindi cha mapumziko cha mwakani watakuwa Marekani.
Huku ni kuchoshana. Wachezaji nao ni binadamu. Wanahitaji kupumzisha miili na akili zao na wanahitaji kuwa karibu na familia zao na hali kadhalika faragha.
Chama cha Ligi za Nchi Duniani (WFL) kimeshamuandikia kaimu katibu mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Mattias Grafstrom kumweleza kuwa kinakusudia kufungua kesi kupinga maboresho ya mashindano hayo kwa maelezo kwamba yanatishia ubora wa afya za wachezaji. Chama nhicho pia kinasema Fifa iliandaa mashindano hayo bila ya kufanya mawasiliano na wadau wake kuhusu motisha wa kifedha utakaotolewa.
Fifa imeahidi kukutana na viongozi wa chama hicho kulijadili suala hilo huku ikishangaa kwamba ligi zinalalamika kuongeza idadi ya mechi wakati Chama cha Soka Ulaya (Uefa) kimeongeza mechi mbili kwa kila klabu kwenye Ligi ya Mabingwa lakini hakilalamikiwi.
Grafstrom pia amemwambia mwenyekiti wa WFL, Richard Masters, ambaye pia ni ofisa mtendaji mkuu (CEO) wa Ligi Kuu ya England, kuwa England pia iliandaa mashindano ya timu sita nchini Marekani mwaka jana, lakini suala la uwingi wa mashindano halikuwa tatizo.
Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (FIFPRO) kimeungana na WFL kuiandikia barua Fifa kuitaka isimamishe mashindano hayo ambayo sasa yamepewa jina la Intercontinetal Cup hadi kutakapofikia makubaliano kuhusu kalenda ya kimataifa ya mechi (IMC).
“Mpango wa sasa wa Fifa wa kuendeleza mashindano yake—kama vile Kombe la Dunia, Klabu Bingwa ya Dunia au Intercontinetal Cup—unavuruga sekta ya mpira wa miguu, kutishia (uhai) wa ligi za nchi na kuathiri afya na hali za wachezaji,” gazeti la The Guardian la Uingereza limenukuu barua hiyo.
Kalenda ya mpira wa miguu imezidi kujazwa na kuongeza ukubwa wa mashindano. Fainali zijazo za Kombe la Dunia zitashirikisha timu 48 kutoka 32 za sasa, wakati mashindano mawili ya klabu barani Ulaya yataongezewa mechi hadi kufikia 36, yaani timu itatakiwa icheze mechi 17 kufika fainali.
Kwa hiyo, si suala la afya za wachezaji pekee, bali pia uhai wa ligi za nchi ambazp zinahitaji muda na wachezaji wenye utimamu wa mwili kuweza kuwa na ushindani na kuvutia watu na kampuni.
Ni katika mukhtadha huo, Baraza la Soka la Afrika Mashariki (Cecafa) lilitakiwa kuangalia kwa makini kabla ya kurejesha mashindano ya Kombe la Kagame yakiwa yamepanuliwa zaidi na mengine yaliyo chini yake.
Cecafa imetangaza kurejesha mashindano hayo yakishiriki timu 16. Yatafanyika kuanzia Julai 20 hadi Agosti 4 yakishirikisha mabingwa wan chi 12 wanachama na timu alikwa nne, ambazo ni mabingwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, TP Mazembe, Azam na Simba.
Pamoja na hoja hiyo kubwa duniani ya afya za wachezaji na kuvurugwa kwa kalenda za mechi za nchi, Cecafa ilitakiwa itambue kuwa mashindano hayo yanaweza yakafanyika bila ya timu shiriki kuwa na vikosi vyake imara kwa kuwa suala la usajili litakuwa bado halijakamilika.
Mbali na kutokamilika, wachezaji wapya wanaosajiliwa na klabu hizo hawatawajibika kuwahi kuripoti kwa wajiri wapya ambao mara nyingi kwa wakati huo huwa wanakusanya wachezaji wao wa timu za vijana wanaoweza kuingizwa kikosi cha kwanza na kuwatumia katika mechi za kirafiki kujiandaa kwa msimu mpya.
Hata mechi za klabu hizo za kufungua msimu huhusisha wachezaji wapya vijana na kwa nadra huonekana wale wachezaji nyota wapya ambao hupewa muda kidogo kwa ajili ya kuwatambulisha.
Na hakuna kanuni zitakazozilazimisha klabu hizi kutuma nyota wake wote, hali inayoweza kupoteza ushindani na hatimaye mvuto na hivyo kurudisha nyuma kampuni ambazo pengine zingetia fedha za matangazo.
Katika mazingira ambayo suala la afya za wachezaji linazidi kuwa muhimu na kalenda kuingiliwa na mashindano mengi yanayoandaliwa na Fifa, Cecafa haina budi kubadili muundo wa Kombe la Kagame ili uwe hauingiliani sana na ligi za nchi na pia uwe ni ule unaoshirikisha timu zilizo kamili na zenye wachezaji wenye utimamu wa mwili.
Kama mashindano hayo yatapangwa vizuri, yanaweza kufanyika kwa mtindo wa ligi wa nyumbani na ugenini kwa kuzingatia kalenda za Fifa, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kalenda za nchi wanachama, ambao wanaweza kukubaliana wiki za Cecafa Football.
Ukiwa na wiki ya Cecafa, maana yake mechi zitakuwa zinachezwa kati ya Ijumaa na Jumapili na kutangazwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki na hivyo kuyapa thamani mashindano.
Yaani vyombo vya habari vya ukanda mzima vitakuwa vinafuatilia mashindano hayo kwa karibu zaidi kila wiki ya Cecafa inapofika tangu msimu unaanza hadi unapomalizika, muda ambao wadhamini hupenda kwa kuwa kwa kujihusisha na mashindano kama hayo yaliyotapakaa katika nchi 12 na kwa karibu miezi tisa, wanapata thamani kubwa zaidi.
Kuendelea kuwa na mashindano katika kituo kimoja yakuyapi thamani ile inayostahili na pale timu za nchi mwenyeji zinapotolewa, huwa n dio mwisho wa mashabiki kwenda viwanjani na hivyo kuwepo na uwezekano fainali kuchezwa kwenye uwanja mtupu, wakati kucheza nyumbani na ugenini kunaihakikishia Cecafa uwingi wa mashabiki katika kila mchezo.
Ni vizuri kwa Cecafa n ahata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufuatilia masuala yanayoendelea duniani ili kunapofanyika maamuzi yawe yamezingatia hoja hizo badala ya kuzipuuza kwa kudhani kuwa masuala hayo bado hayajafika ukanda au nchi husika.