Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu amesema kampuni hiyo kwa sasa imejikita zaidi kwenye utengenezaji wa maudhui ya kidijitali kupitia mitandao yake ya kijamii.
Amesema huo ni mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa miti imekuwa ikitumika kutengeneza karatasi ambazo ni bidhaa inayotumika kuzalisha magazeti.
Hata hivyo, amesema ingawa bado MCL inaendelea kuchapisha magazeti imepata miongozo zaidi ya 17 kupitia harakati za maendeleo endelevu.
“Tunatumia bidhaa zinazotokana na miti kutengeneza karatasi, tulifikiria ni nini tunafanya kupata malighafi muhimu tukaamua kuchukua hatua za makusudi kuwa suluhisho.
“Tukapata miongozo ya kutosha kupitia harakati za maendeleo endelevu zipatazo 17. Hivi karibuni Rais amekuja na kampeni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, nasi tukaangalia kuona tunafanya nini kuchangia hili,” amesema wakati akizungumza kwenye Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi linalofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo Ijumaa, Juni 14, 2024.
Mgeni rasmi kwenye kongamano hilo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Sulemain Jafo aliyewakilishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza.