Makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja yamepatikana – DW – 14.06.2024

Makubaliano hayo yametokana na mazungumzo ya ushirikiano baada ya ANC kushindwa kupata viti vya kutosha bungeni katika uchaguzi uliofanyika mwezi Mei.  

Akizungumza usiku wa kuamkia leo, Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula, amesema serikali itakuwa ya sera za mrengo wa kati baada ya vyama vya mrengo mkali wa kushoto kukataa mazungumzo ya kujiunga na serikali.

Mbalula aliuambia mkutano na waandishi habari kwamba wamepata makubaliano chini ya msingi wa pande zote kuridhia haja ya kufanya kazi pamoja.

Makubaliano hayo yumkini yatawezesha Rais Cyril Ramaphosa kuchaguliwa kwa muhula wa pili wakati bunge jipya litakapofanya kikao cha kwanza baadae leo mjini Cape Town.

Mbalula ameuelezea muungano uliopatikana kuwa utaunda serikali ya umoja wa kitaifa na utavijumuisha vyama vya Democratic Alliance (DA), Chama kinachopigania maslahi ya jamii ya Wazulu cha Inkatha Freedom (IFP) na vyama vingine viwili vidogo kile cha mrengo wa kati kushoto cha United Democratic Movement na cha mrengo mkali wa kulia cha Afrikaner Freedom Front Plus (FF+).

EFF na uMkhonto weSizwe kutokuwa sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa

Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula
Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula.Picha: AP Photo/picture alliance

Mbalula amesema  chama cha mrengo mkali wa shoto Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na mwanasiasa machachari Julius Malema hakikushirikishwa kwenye mazungumzo baada ya mashauriano na kiongozi wake kutozaa matunda. 

Kadhalika chama cha uMkhonto weSizwe (MK) kinachoongozwa na Rais wa zamani Jacob Zuma nacho hakitoshiriki serikali hiyo kwa sababu kinaupinga muungano huo.

Chama hicho kilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi uliopita kikiwa kimejinyakulia vita 58 vya bunge. Mbalula amesema mazungumzo na chama hicho yataendelea lakini viongozi wake wanayapinga matokeo ya uchaguzi na wanapanga kuwaelekeza wabunge wake wateule kususia vikao vya Bunge.

Kwa miaka 30 tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi na utawala wa wazungu wachache chama cha ANC cha hayati Nelson Mandela kilikuwa kikishinda wingi wa vita bungeni na kukiwezesha kuunda serikali chenyewe.

Hata hivyo katika uchaguzi wa Mei 29 kikiwa kimetiwa doa na mfululizo wa kashfa za rushwa na uchumi unaochechemea, ANC iliambulia asilimia 40 pekee ya kura na kupata viti 159 vya wabunge kati ya 400 vya Bunge la Taifa.

Umahiri wa ANC kisiasa ndiyo umefanikisha makubaliano hayo? 

Chini ya katiba ya Afrika Kusini, rais huchaguliwa na wabunge kupitia kura ya siri. Kufanikiwa kwa ANC kuvishawishi vyama vingine kuunda serikali ya pamoja ikiwemo kile kilichokuwa chama kikuu cha upinzani cha DA kumedhihirisha uwezo wa chama hicho katika kuzichanga karata zake vizuri kisiasa.

Afrika Kusini | Cyril Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa huenda atachaguliwa tena kuongoza Afrika Kusini.Picha: Chris McGrath/Getty Images

Kwa lugha rahisi serikali ya umoja wa kitaifa hujumuisha muungano mpana mpana wa vyama vinavyojumuika kuunda serikali.

Unaweza kujumuisha vyama vyote vilivyo na uwakilishi bungeni au angalau vyama vyote vikubwa na kuvipa nafasi ya kuwa sehemu ya utawala wa nchi. 

Serikali ya aina hiyo huwa na miundo tofauti. Afrika Kusini inayo historia ya kuwa na serikali hiyo iliyoundwa baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliofanyika mwaka 1994.

Wakati huo kiongozi wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi na utawala wa wazungu wachache Nelson Mandela alichaguliwa kuwa rais na serikali ilikuwa ikiendeshwa chini ya katiba ya mpito. 

Wengi watasubiri kwa shauku kuona iwapo Ramaphosa atachaguliwa rasmi na bunge kuanza muhula wa pili na jinsi serikali hiyo mpya ya umoja wa kitaifa itakavyoundwa.

Related Posts