Mboya ashindwa kutetea Uenyekiti wa Chadema Moshi Mjini, Mlay ashinda

Moshi. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Moshi Mjini, Raymond Mboya ameshindwa kutetea nafasi yake, baada ya wajumbe kumchagua, African Mlay.

Mwenyekiti wa Uchaguzi Antony Ndewawio amemtangaza Mlay kuwa Mwenyekiti wa Chadema Moshi Mjini kwa kupata kura 120, huku Mboya aliyepata kura 93.

Kwa upande wa Katibu wa Chadema Jimbo la Moshi Mjini, alimtangaza Zephania Kisambu aliyepata kura 108 dhidi ya John Minja aliyepata kura 106.

Katibu Mwenezi amechaguliwa Mohamed Ally kwa kura 147 dhidi ya mpinzani wake Stiven Ngasa aliyepata kura 70, Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa amechaguliwa Collins Tamimu, huku wajumbe wa kamati tendaji wakichaguliwa Suzy Kilawe, Ester Kalikawe, Deogratius Kiwelu na Dominick Tarimo na  nafasi ya mweka hazina akichaguliwa Sezari Kimario.

Akizungumza  jana Juni, 13 2024 Mboya alipopewa nafasi ya kushukuru, Mboya amewaomba wajumbe kuvunja makundi yaliyokuwa katika uchaguzi na kuunganisha nguvu pamoja kupambana na adui yao ambaye ni Chama cha Mapinduzi (CCM).

Pia, amewataka waliokuwa timu yake katika uchaguzi, wasiumie kwa lolote kwa kuwa wamefanya kupokezana kijiti na mwenzake ili kuendelea pale alikoishia na watashirikiana kuhakikisha Chadema inasonga mbele.

“Nimpongeze mwenyekiti aliyeshinda, tumeingia hapa tukiwa na makundi, lakini tukitoka hapa, adui yetu ni CCM, niwaombe viongozi, tutoe ushirikiano kwa uongozi mpya wa chama wa wilaya na mimi na wengine ambao kura hazikutosha tutashirikiana, kwa kuwa adui yetu ni CCM,”amesema Mboya ambaye ni Meya wa zamani wa Manispaa ya Moshi.

 “Tuna kazi kubwa sana mbele yetu, tuliyokuwa nayo sisi ‘tutashea’ na wewe na kukupa mipango tuliyokuwa nayo kamati tendaji ili ‘ uchanganye na ya kwako na kamati tendaji yako tuvuke salama.”

Mlay aliyechaguliwa kwa kura  kuwa mwenyekiti, amewataka wajumbe kuvunja makundi na kushirikiana kwa pamoja kufanya kazi ili kuivusha Chadema katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani 2025.

“Niwashukuru kwa kuona katika nafasi hii ninatosha, ninachoomba kwenu ni ushirikiano. Viongozi wa kamati tendaji wote tuliochaguliwa, tukafanye kazi, tusibweteke, tukakae kama timu kufanya kazi, hatutakuwa na mchezo, tunakwenda kufanya kazi,”amesema Mlay.

“Hakuna tena makundi, hakuna tena kundi la Afrikan wala la Ray Mboya, tuwe timu moja tukafanye kazi kuhakiksha tunashinda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na hata katika uchaguzi mkuu.”

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila amewataka wote waliochaguliwa kwenda kufanya kazi  ya kukijenga chama hicho na kuhakikisha wanashinda katika chaguzi zilizopo mbele.

“Msiende mkatundika makoti ofisini, nendeni mkafanye kazi ya kujenga chama Manispaa ya Moshi, nitawashangaa sana kama hatutachukua Serikali za mitaa kama hatutachukua madiwani, mbunge na Rais mwaka 2025,”amesema Kilawila.

Related Posts