MCL yajikita kuhamasisha uelewa wa  mabadiliko ya tabianchi kidijitali

Dar es Salaam.  Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imeahidi kuendelea kutoa maudhui katika kuhamasisha uelewa wa mabadiliko ya tabianchi kidijitali.

Haya yalielezwa na Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Victor Mushi kwenye Kongamano la Jukwaa la Fikra linalowakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira kujadili changamoto za mabadiliko ya tabianchi. 

Jukwaa hili linajadili mada isemayo: “Safari kuelekea mustakabali wenye urafiki na mazingira” ikiwa na lengo ni kuleta suluhu ya pamoja na endelevu kwa mustakabali wa nchi kwenye changamoto za kimazingira.
Mushi amesema kampuni hiyo ilianza safari ya kuelekea mustakabali wenye urafiki na mazingira kupitia mijadala ya mabadiliko ya tabianchi mwaka jana.

“Ni vizuri kwetu tukazungumzia masuala ya usalama wa chakula na uchumi himilivu kwa kuwezesha Watanzania kupata maudhui kupitia mitandao yetu ya kijamii na magazeti ya Mwananchi na The Citizen,” amesema Mushi.

“Tumeendelea kuzalisha maudhui yenye kuelimisha juu ya mabadiliko ya tabianchi na athari zake.
 Zaidi tunalenga kuwafikia Watanzania wengi kupitia dijitali, ndio maana tumeweka nguvu kubwa kutoa habari zetu kwa njia hii.

“Nawaahidi wote mliohudhuria mkutano huu mtapata ufikiaji wa maudhui ya mitandao yetu bure kwa muda wa wiki moja. Kwenye tovuti zetu yapo baadhi ya maudhui ambayo ni ya kulipia,” amesema Mushi.

Mushi amesema kampuni inatambua kuwa usomaji wa magazeti mtandaoni unasaidia kupunguza uchafuzi na athari kwa mazingira kwa kuwa magazeti yanazalishwa kutoka kwenye miti.

Related Posts

en English sw Swahili