WALIMZIKA Sir Bobby Charlton Oktoba mwaka jana katika makaburi ya Manchester. Miaka 30 kabla ya hapo walikuwa wamemzika Sir Bobby Moore katika makaburi ya London mwaka 1993. Nawazungumzia watu wanaoitwa Waingereza walivyoondokewa na mashujaa wao katika soka.
Miongoni mwa wachezaji wa mwisho mwisho kufariki katika kikosi chao kilichotwaa Kombe la Dunia ni huyu Sir Bobby Charlton. Kuanzia pale kwa Moore hadi Charlton Waingereza wamebakisha mchezaji mmoja tu ambaye yupo hai katika kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia katika ardhi yao mwaka 1966 pale Wembley.
Amebakia Sir Geoff Hurst tu. Wengine wote wamekwenda. Kabla ya hapo na baada ya kombe lile Waingereza hawajawahi kutwaa kombe lolote kubwa la soka. Linabakia lile tu, basi. Miaka 58 sasa. Vizazi na vizazi vimezaliwa na havijawahi kuona Waingereza wakitwaa kombe lolote kubwa. Ukweli unaoumiza.
Watu wachache duniani wamebaki hai tangu waliposhuhudia England wakitwaa taji lolote kubwa. Na hao ambao wamebaki hai kwa sasa wengi kati yao wanauguza ugonjwa wa kupoteza fahamu (dementia). Hata Sir Geoff Hurst mwenyewe ambaye alifunga hat-trick katika fainali hiyo ya 1966 katika ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Ujerumani Magharibi naye anaugua dementia.
Ninekumbuka yote haya baada ya kuifikiria michuano ya Euro ambayo imeanza jana pale Ujerumani. Waingereza wamo kama kawaida yao. Wamesafiri kwa mbwembwe kwenda Ujerumani kama kawaida yao. Wana uwezo wa kutupa kumbukumbu yoyote sisi ambao hatukuwapo duniani wakati kina Bobby Charlton wakichukua taji pekee la Uingereza katika soka?
Aibu iliyoje. Waingereza hawajawahi kutwaa Euro. Mataifa mengi makubwa Ulaya yamewahi kutwaa Euro. Wao hadi sasa hivi vimebadilika vizazi vingi, lakini hawajawahi hata kutwaa Euro. Hawajawahi kurudi tena katika pambano la fainali la Kombe la Dunia. Hawajawahi kucheza pambano lolote la fainali za Euro.
Wanakwendaje katika Euro? Hawajaenda kwa kelele sana, lakini wana vipaji maridhawa. Kwangu mimi ni pengine kuliko wakati mwingine wowote tangu niwafahamu. Najua utanibishia. Una haki. Wamewahi kuwa na wachezaji wenye majina makubwa hapo kati na hivi karibuni. Kina Steven Gerrard, kina Frank Lampard, kina Wayne Rooney na wengineo.
Lakini subiri kwanza. Nadhani walikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza kwa mifumo, kucheza kwa misingi waliyofundishwa. Wachezaji wanaocheza kwa nidhamu zaidi ya soka. Hata hivyo, kwa sasa nadhani nawashuhudia Waingereza wenye vipaji zaidi. Mchezaji mmoja mmoja anaweza kuuchukua mpira na kuuchezea zaidi kuliko zamani.
Zaidi ya kila kitu, hawana first eleven pekee. Wana wachezaji wengi katika nafasi nyingi. Labda ndipo ilipokuja jeuri ya kumuacha mchezaji kama Jack Grealish ambaye kwa sasa analewa zake Dubai. Hauwezi kumbishia sana Gareth Southgate kwa sababu ana vipaji vingi.
Kyle Walker sio Gary Neville. Ni fundi. Phil Foden fundi. Bukayo Saka fundi. Jarrod Bowen fundi. Kebbie Mainoo fundi. Cole Palmer fundi. Kila maeneo naona mafundi. Trent Alexander Arnold fundi. Declan Rice, mapafu ya mbwa halafu fundi mkubwa. John Stones, unachezaje timu ya Pep Guardiola kama hauna ufundi wowote mguuni. Ni fundi hasa. Mpange kama beki wa kati, mpange kama kiungo, anabakia kuwa fundi tu.
Mbele wana wafungaji watatu. Harry Kane, Ollie Watkins na Ivan Toney. Wote hawa wanaweza kukufunga muda wowote ambao utafanya kosa la kuwapa nafasi. Achana na Harry Kane, Erling Haaland na Roberto Lewandowski, daraja zuri la washambuliaji linalofuata ni hili la kina Ivan Toney, hasa katika zama hizi ambazo dunia ina uhaba mkubwa wa washambuliaji.
Halafu kuna Jude Bellingham. Mtu na nusu. Katika umri wa miaka 20 tu majuzi Toni Kroos alikuwa anajiuliza kama Jude alikuwa anasema kweli kuhusu umri wake. Kisa? Namna alivyopevuka katika aina yake ya mchezo. Ni zaidi ya mchezaji wa kawaida. Tumewadharau Waingereza kwa muda mrefu, lakini hata Wahispaniola pale Santiago Bernabeu walimpa jezi ya Zidane Zidane. Jezi namba 5.
Nini kinafuata? Umefika muda kwao kuacha alama nyingine. Imechosha kila siku kusikia namna ambavyo wanazungumzia ubingwa wao wa Kombe la Dunia 1966. Kitu kibaya zaidi ni kwamba hata watunza kumbukumbu wa kilichofanyika pale Wembley mwaka 1966 nao wanafariki. Waingereza wanahitaji kumbukumbu nyingine ya kutupigia kelele.
Wakati haya yakitokea, kama ukipima sana basi hauoni timu nyingi za kuwasumbua Waingereza kwa maana ya mchezaji mmoja mmoja, au timu wanazocheza, au namna ambavyo baadhi ya mataifa ya Ulaya yameshuka kisoka. Unaweza kuwadharau Waingereza lakini wana wachezaji kadhaa kutoka Manchester City, Arsenal, Liverpool, Bayern Munich, Manchester United pia. Halafu wana Jude kutoka Real Madrid.
Tishio kubwa kwao linaweza kutoka kwa Wafaransa ambao wanaongozwa na Kylian Mbappe. Na achana na Kylian lakini wana wachezaji wengine wengi wakubwa wanaotoka timu kubwa. Wafaransa licha ya kwamba hawakutetea Kombe la Dunia pale Doha 2022 baada ya kutwaa taji la Moscow 2018 bado wanapitia katika kizazi cha mafundi ambao wengi ni watoto wa wahamiaji kutoka Afrika.
Wengine ambao ni tishio ni Wajerumani. Angalia Borussia Dortmund walipofika katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Tazama Bayern Munich walipoishia. Halafu jumlisha kina Antonio Rudger, Kai Havert, Toni Kroos na wengineo. Jumlisha na ukweli kwamba ni taifa ambalo lina nidhamu kubwa kisoka na mafanikio makubwa duniani kwa ujumbe.
Halafu kuna mataifa ambayo yanakuja na kuondoka. Yanaleta kizazi cha dhahabu na kuondoka. Ndio hawa kina Uholanzi na Ubelgiji. Sio tishio sana kwa Muingereza kama utahesabu uwezo wa mchezaji mmoja mmoja kwa sasa au kihistoria kama utatazama mafanikio yao kwa ujumla. Walau Waingereza wametwaa Kombe la Dunia mara moja kuliko Uholanzi na Ubelgiji ambao hawajafanya hivyo.
Kevin De Bruyne anamaliza na kizazi chake cha dhahabu akiwa hana taji lolote lile. Amejikuta hadi akiingiliana na kizazi kipya wakati wenzake kina Eden Hazard wakiwa wanakunywa bia za pensheni. Nadhani hii itakuwa michuano yake ya mwisho. Baada ya hapo atastaafu. Hata michuano ya Kombe la Dunia pale Marekani, Mexico na Canada inaweza kumkuta akiwa Saudi Arabia.
Na sasa acha tuwatazame Waingereza wanaweza kufanya nini katika michuano hii. Wana vijana wengi wenye ubora mwingi. Wanaweza kukosea hapa lakini bado wakarekebisha mambo Amerika Kaskazini ambako Kombe la Dunia litachezwa 2026. Hata hivyo, kipimo chao kikubwa ni michuano hii. Na sio tu kipimo cha maandalizi ya Kombe la Dunia lijalo bali pia kipimo cha kuokoa aibu ambayo Waingereza wamekabiliana nayo kwa miaka mingi tangu kina Sir Bobby wawili, Charlton na Moore walipotwaa Kombe la Dunia pale Wembley mwaka 1966.
Waingereza pia wana utawala mpya wa Kifalme. Malkia Elizabeth baada ya kushuhudia ule ubingwa wa mwaka 1966 hakuweza kupewa pumzi tena za kushuhudia ubingwa mwingine. Hata vizazi vyake havikupata bahati hiyo. Sasa hivi mwanae Charles ni mfalme. Hadithi itabakia ile ile au anaweza kuwa ameingia na bahati yake?