Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amefanya uteuzi wa kamishna na wakurugenzi katika wizara na taasisi za Serikali.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Ijumaa Juni 14, 2024 na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Zena Said inamtaja Omar Said Omar kuteuliwa kuwa Kamishna wa Usimamizi wa Sera za Ununuzi wa Umma katika Ofisi ya Rais Fedha na Mipango.
Kabla ya uteuzi huo, Omar alikuwa Mkurugenzi wa Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri katika Mamlaka ya Ununuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma (ZPPDA).
Suleiman Saleh Haji ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ZPPDA, awali alikuwa Meneja wa Ununuzi Kampuni ya Maendeleo ya Petroli Zanzibar (ZPDC).
Rajab Uweje Yakoub ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, awali alikuwa Ofisa Mwandamizi na Utawala ofisi hiyo hiyo.
“Makame Salum Ali ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara Mipango, Sera na Utafiti Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Mwandamizi Tume ya Mipango ya Zanzibar,” inaeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi unaanza leo Ijumaa Juni 14, 2024.