Na Mwandishi Maalumu –
Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 900 kwaajili ya kuwasaidia watoto
wenye matatizo ya moyo wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu.
Fedha hizo zimelenga kuwagharamia watoto wenye magonjwa ya
moyo ambayo ni magumu kufanyiwa upasuaji ambao wamekuwa katika foleni ya
kusubiria matibabu katika Taasisi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni jijini
Dar es Salaam Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Angela Muhozya alisema fedha hizo zitatumika kuwafanyia upasuaji wa
kufungua kifua watoto 30 matatibu yatakayotolewa kwa kipindi cha wiki mbili na
wataalamu wa Taasisi hiyo.
“Tunashukuru tangu tumeanza kambi hii imekuwa ya mafanikio kwani
upasuaji tunaoufanya ni mkubwa kwa watoto, kupitia kambi hii pia tumeweza
kumfanyia upasuaji mtoto mwenye uzito wa kilo mbili na upasuaji wake
umefanikiwa”, alisema Dkt. Angela.
Dkt. Angela alisema matibabu yanayotolewa kwa watoto hao 30
ni makubwa kwani watoto wana changamoto zaidi ya moja zinazopelekea mahitaji ya
vifaa tiba na dawa kuwa makubwa na kuyafanya matibabu hayo kuwa na gharama
kubwa.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo
wake wa kujitoa kwaajili ya watoto hawa ambao wanapata huduma katika Taasisi
yetu”, alisema Dkt. Angela.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felix Shonyela alisema kambi hiyo
inatoa huduma kwa watoto wenye matatizo magumu na wale wenye shida zaidi ya
moja kwenye mioyo yao.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji
wa moyo watoto hawa wataendelea kufanya shughuli zao kama kawaida na shida
waliozokuwa wanapata mwanzo zitaondoka na kuwa vizuri kama watoto wengine”,
alisema Dkt. Shonyela.
Dkt. Shonyela alitoa wito kwa wazazi wenye watoto wanapoona
watoto wana dalili za kuchoka, vidole kuvimba, kuwa na rangi ya bluu kwenye
vidole na midogo pamoja na ukuaji hafifu kuwafikisha JKCI mapema kwaajili ya
uchunguzi kwani watoto wengi wamekuwa wakicheleweshwa na kupelekea baadhi ya
matibabu kushindwa kufanyika.
Naye mzazi wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo
Prisca Theophil alimshukuru Rais Samia kwa kuwasaidia watoto wenye matatizo ya
moyo wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi akiwemo mtoto wake.
Prisca alisema aligundua mtoto wake ana tatizo la moyo mwaka
2022 na kuanza kupatiwa matibabu JKCI lakini hakuwa na uwezo wa kulipia gharama
za upasuaji kutokana na kipato chake kuwa kidogo.
“Namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuwasaidia watoto
wetu, mwanangu alikuwa na tundu kwenye moyo, matatizo ya valvu na tatizo la
mishipa ya damu kupitia fedha za mama Samia amefanyiwa upasuaji na sasa
anaendelea vizuri”, alisema Prisca.