Serikali yawataka Wandishi wa Habari kuelimisha jamii Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imewataka Waandishi wa Habari nchini kutambua nafasi yao muhimu katika kuelimisha jamii ili kushiriki kikamilifu katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Akizungumza leo, Juni 14, jijini Dar es Salaam, katika semina iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, aliwaeleza waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini umuhimu wa jukumu lao.

“Vyombo vya habari vina ushawishi mkubwa katika jamii. Ukiona jamii ya sasa, wanachozungumza na wanachojadiliana kwa kiasi kikubwa kinatokana na ushawishi wa vyombo vya habari,” alisema Mhandisi Kisaka.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wanahabari kuwa na weledi na kufuata maadili katika taaluma yao ili kuhakikisha umma unajisikia faraja na kushiriki katika maboresho ya daftari bila kusita. Pia alisema kuwa vyombo vya habari vinaunganisha jamii katika masuala ya kitaifa na kuchochea maendeleo.

“Nawataka wanahabari kutambua kuwa wao ni watoa huduma katika jamii na huduma inayotolewa inatambulika kuwa ni haki ya msingi kiraia na haki ya kila mtu,” aliongeza.

Mhandisi Kisaka alieleza kuwa sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 inatambua sekta hiyo kama huduma muhimu kwa jamii. “Idadi ya watu wanaofikiwa na utangazaji wa televisheni kwa njia ya setelite (DTH) ni asilimia 100, na wale wanaofikiwa na utangazaji wa televisheni kwa kutumia miundombinu ardhini (DTI) ni asilimia 56. Idadi ya visambuzi ni milioni 3.8,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa hadi kufikia Machi 2024, idadi ya watumiaji wa simu janja imeongezeka kufikia asilimia 32.59 kutoka asilimia 32.13 iliyorekodiwa Disemba 2023.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Patrick Lupangula, aliwahimiza wanahabari kutoa habari za kweli kwa umma wakati wote wa uchaguzi. “Kupotosha taarifa kunaweza kusababisha hofu, kuchochea ghasia na kupunguza imani ya wananchi kwenye mchakato wa uchaguzi,” alisema Lupangula.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Patrick Lupangula.

Alisisitiza umuhimu wa usawa na haki kwa wagombea wote na vyama vyote vya siasa, pamoja na kufuata kanuni, sheria, na maadili ya habari.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mtibora Seleman, alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa pamoja katika kusukuma maendeleo ya Taifa kupitia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Tume itaendelea kuhamasisha wananchi ili wajitokeze kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha ili waweze kupata haki zao za kikatiba,” alisema Mtibora.

Related Posts