MABOSI wa Simba wameanza mazungumzo ya kumnasa kiungo mkabaji raia wa Guinea, Mohamed Damaro Camara.
Damaro anayeichezea Hafia ya Guinea aliyojiunga nayo mwaka 2020 akitokea Milo FC, ameonyesha nia ya kujiunga na Simba jambo linalorahisisha dili la nyota (22) anayecheza pia beki wa kati.
KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda inadaiwa yupo mbioni kurejea Coastal Union kwa nia ya kwenda kuiongezea nguvu timu hiyo itakayoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Inaelezwa Mgunda anatakiwa na Coastal kwa uzoefu alionao anga za kimataifa ili asaidiane na David Ouma na inadaiwa mazungumzo yapo mahali pazuri na muda wowote inaweza kutangazwa kurejea kwa Mgosi kwa Wagosi.
KLABU ya Coastal Union imeanza mazungumzo ya kumpata mshambuliaji wa Tabora United, Mcongoman, Lumiere Banza Kalumba kwa ajili ya msimu ujao.Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Tabora Utd mwanzoni mwa msimu akitokea TP Mazembe, huenda akaachana na kikosi hicho ikiwa kitashindwa kubaki Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao, jambo linalowafanya mabosi wa Coastal kuwania saini yake.
UONGOZI wa Simba unafuatilia kwa ukaribu huduma ya beki wa kushoto wa KMC, Rahim Shomary ili kuongeza nguvu katika timu hiyo.Shomary mwenye miaka 19, ndiye mchezaji mdogo zaidi katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita aliyechangia mabao mengi akiwa na sita, akifunga moja na kuasisti matano, hivyo kuwafanya mabosi wa Simba kumuwania. Daudi Elibahati.
KLABU ya Tanzania Prisons, imeanza kuiwinda saini ya mshambuliaji wa TMA, Ramadhan Salum Chobwedo kwa ajili ya msimu ujao.Nyota huyo msimu uliopita akiwa na kikosi cha TMA katika Ligi ya Championship, alifunga mabao matano na kuasisti 12 jambo linalowafanya maafande hao wa Mbeya kuvutiwa kuhitaji saini yake ili kuiongeza nguvu timu hiyo.
INAELEZWA kuwa straika wa Fountain Gate Princess, Amina Ramadhan yupo katika mazungumzo na klabu ya JKT Queens kwa ajili ya kuwatumikia msimu ujao.
Dirisha llilopita la usajili klabu hiyo ilifikia pazuri dili hilo liliingia doa baada ya Simba Queens kuamua kumrejesha Jentrix Shikangwa Msimbazi.
YANGA Princess imeanza mazungumzo na kingo mshambuliaji wa Amed S.K ya Uturuki, Mtanzania Diana Msewa ambaye yuko mbioni kumalizana na klabu hiyo.
Inaelezwa kuwa endapo Yanga itamnasa Diana basi itaachana na dili la kiungo wa JKT Queens Amina Bilal ambaye wana uwezo sawa wa kucheza.