TFF yakunjua makucha Ligi Kuu ya Wanawake

TIMU ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), Ceasiaa Queens imelimwa faini ya Sh 2 milioni na baadhi ya maofisa na wachezaji wa timu hiyo kuadhibiwa kwa kosa la kufanya vurugu na kuvunja pambano la ligi hiyo iliyokuwa imeshinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Alliance Girls.

Pambano hilo lililopigwa Juni 11, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Ceasiaa ilishinda mabao 2-1, lakini ilivunja pambano dakika ya 88 wakati mwamuzi Agneta Issack kutoka Kagera kuashiria penalti kwa wenyeji Alliance na maofisa wa timu wageni walimvamia na kumpuga mwamuzi huyo na pambano kuvunjika.

Jana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitoa taarifa ya Kamati ya Soka la Wanawake kuinyang’anya ushindi Ceasiaa na kuizawadiwa Alliance pointi tatu na mabao matatu, huku ikiilima klabu hiyo Sh 2Milioni kwa mujibu wa kanuni ya 33 (1) na 33(6) za Kanuni za WPL.

Pia kamati hiyo, imemfungia kwa muda wa miezi sita na faini ya Sh500,000 kila mmoja, Meneja wa timu hiyo,Tedson Haule, meneja msaidizi, Jumanne Musuba, Kocha wa Makipa, Bashir Twalib na mchezaji, Khadija Mwita kwa kuhusika na vurugu za kumshambulia mwamuzi huyo.

Kwa uamuzi huo, Alliance imefikisha pointi 13 (kabla ya mechi za jana) na mabao 18 ikifungwa 41 ikisalia nafasi ya tisa kati ya timu 10, wakati Ceasiaa imepunguzwa pointi kutoka 32 hadi 29, ikisalia  nafasi ya nne sasa (hii ni kabla ya mechi za kufungia msimu zilizochezwa jana na Simba kupewa kombe ililolitwaa).

Simba ilikuwa uwanjani jana kuvaana na Geita Queens na mchezo huo kutumika kukabidhiwa taji lake, huo ni ubingwa wa nne kwa timu hiyo tangu Ligi Kuu ya Wanawake ilipoasisiwa mwaka 2015 na aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi, huku bingwa wa kwanza akiwa ni Mlandizi Queens kisha JKT Queens kulitwaa mara mbili mfululizo, 2017-2018 na 2018-2019.

Simba ilibeba taji hilo mara tatu mfululizo kuanzia 2019-2020, 2020- 2021 na 2021-2022 na msimu uliopita JKT ilirejesha ubingwa huo kabla ya msimu huu Simba kufanya kweli.

Kubeba ubingwa huo, Simba imekata tiketi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika ikiwa ni mara ya pili kwake baada ya msimu uliopita ilimaliza ya nne kwa kufika nusu fainali.

Msimu huu JKT ilienda kushiriki michuano hiyo na kutolewa hatua ya makundi.

Katika hatua nyingine TFF imetangaza kufunguliwa kwa dirisha la usajilikwa timu za Ligi Kuu Bara, Ligi ya Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) linafunguliwa rasmi leo kama Mwanaspoti lilivyowajulisha jana.

Tofauti na msimu uliopita, safari hii dirisha hilo litafungwa Agosti 15, siku chache kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara Agosti 18 itakayotanguliwa na mechi za Ngao ya Jamii zitakazochezwa kati ya Agosti 8-11 ikishirikisha klabu za Simba walio watetezi, Yanga, Azam na Coastal Union zilizomaliza ndani ya Nne Bora.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo ni kwamba dirisha dogo la msimu huo mpya litafunguliwa Desemba 16 mwaka huu na kufungwa Januari 15 mwakani.

Pia TFF imezikumbusha klabu zitakazoshiriki michuano ya kimataifa kwa msimu ujao kuwa leo Juni 15 ndio mwisho wa usajili wa Leseni za Klabu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Yanga na Azam zenyewe zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kumalizana nafasi mbili za juu, huku Simba na Coastal Union zitashiriki Kombe la Shirikisho zikiwa zimeshika nafasi ya tatu na nne ya msimamo wa Ligi Kuu Bara iliyomaliozika hivi karibuni.

Katika msimu huu Simba na Yanga zilizocheza Ligi ya Mabingwa ziliishia robo fainali, huku Azam na Singida Fountain Gate zikitolewa mapema Shirikisho.

Related Posts