Dar es Salaam. Kutokana na idadi kubwa ya watoto kukosa elimu ya masuala ya haki za binadamu, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umeanzisha jukwaa la watoto watetezi.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alipokuwa akizindua jukwaa hilo jijini hapa litakaloenda na shamrashamra za kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16 mwaka huu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Olengurumwa amesema kuanzishwa kwa jukwaa hilo kutasaidia watoto kujua haki zao na mwisho wa siku iwe rahisi kujitetea pale zinapominywa.
“Mfano sasa hivi tumeshuhudiwa uwepo wa matukio ya ulawiti na ubakaji, yote hii ni kutokana na watoto wetu kutojua haki zao na nini wanapswa kufanya zinapokiukwa,” amesema Olengurumwa.
Katika kuhakikisha elimu hiyo ya utetezi inaendelea, amesema kila mwaka wa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika watakuwa na mdahalo mkubwa wa watoto watakaozungumzia masuala yanayohusu haki zao.
Kwa upande wao, watoto akiwamo mwenyekiti wa Baraza la Watoto wa Afrika, Eunice Deogratius ameitaka jamii kuwapenda watoto na kuwapa haki zao ikiwemo elimu.
Mtoto mwingine, Mephadelly Mrisho amesema wanaokiuka haki za watoto wanapaswa kujua kwamba wana haki kama wao na kwa wale ambao wamekuwa wakizikiuka wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria bila kuonewa aibu ili iwe fundisho na kwa wengine.
Sylivia Rwambo, Mwenyekiti Jukwaa la Haki za Watoto, amesema katika maadhimisho ya mtoto wa Afrika mwaka huu kaulimbiu ni “Elimu kwa watoto wote wa Afrika na wakati ni sasa.”
Kupitia kaulimbiu hiyo, Sylvia ametaka wazazi na walezi kutobweteka na elimu bila ada na badala yake washiriki katika kuchangia gharama nyingine zinazohitajika ili watoto wao waweze kupata elimu.
“Kuna wazazi na walezi baada ya kuambiwa elimu ni bure hawajishughulishi, hii sio sawa kwa kuwa Serikali haiwezi kufanya kila kitu ni lazma nao wachangie kidogo.
“Pia, mamlaka zinazosimamia elimu zinapaswa kuendelea kutoa elimu kuieleza jamii elimu bila ada inamaanisha nini huku kwa wale wasiokuwa na uwezo kabisa kuwekwe taratibu wa kuwasaidia ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa katika safari ya kupata elimu.”
Sylivia ametumia nafasi hiyo kuikumbusha jamii kuwa ulinzi wa mtoto ni wajibu wa kila mwanajamii na kuitaka kuhakikisha inawalinda kwa madhila yoyote yale.