Tozo ya gesi ya magari changamoto, Bunge laombwa kuiondoa

Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kutaka kukusanya Sh9.5 bilioni kutoka kwa watumiaji wa magari yatumiayo gesi asilia iliyokandamizwa (CNG) imeibua mjadala, wasiwasi ukiwa ni kuzorotesha kasi ya watu wanaohama kutoka katika matumizi ya mafuta ambayo bei yake imekuwa na changamoto lukuki.

Tangu kuanza kwa vita ya Russia na Ukraine na baadaye changamoto ya uhaba wa Dola ya Marekani katika mataifa mengi bei ya nishati ya mafuta imekuwa ikipaa kiasi kilichosukuma Serikali kuhamasisha watumiaji wa vyombo vya moto kuhamia kwenye CNG kwa kuwa inapatikana nchini, haiathiriwi na changamoto za nje na bei yake ni nafuu.

Hata hivyo, katikati ya hamasa hiyo na ongezeko la mwamko wa watu kuhamia katika matumizi ya CNG Serikali imetangaza kuanzisha tozo ya Sh382 kwa kila kilo moja ya CNG inayowekwa kwenye magari, kwa kile ilichoeleza ni kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Barabara.

“Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayotumika kufanya matengenezo ya barabara pamoja na kuleta usawa kwa kuwa magari yanayotumia mafuta tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara,” alisema Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipowasilisha bajeti ya Serikali bungeni juzi.

Dk Mwigulu akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 aliongeza kuwa fedha itakayopatikana kwenye tozo hiyo itapelekwa katika Mfuko wa Barabara hatua hiyo ikitarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh9.5 bilioni.

Katika uchambuzi wa bajeti uliofanywa jana na kampuni ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Ernst & Young (EY), Mkurugenzi Mkuu wake, Joseph Sheffu amesema ni muhimu Bunge katika mjadala wa bajeti likaangalia eneo la CNG kwa kina.

Amesema ni kweli kodi inaleta usawa wa tozo ya barabara ambayo kwa sasa wanaotumia magari yanayotumia mafuta wanailipa, lakini CNG inatoa suluhu hadi ya utunzaji wa mazingira kwa kuwa ni nishati safi kuliko mafuta.

“Mapato yanayolengwa siyo mengi na ambao wanatumia CNG kwenye magari ni wachache na kwa ongezeko hili la gharama huenda kasi ya wanaobadilisha mfumo ikapungua kwa kuwa ataona gharama yake ni kama mafuta, pengine tungesubiri kwanza watu wawe wengi ndipo tutoze,” amesema Sheffu.

“Serikali sijui inataka nini, bei ya mafuta imekuwa kubwa wakatuhimiza tuhamie kwenye gesi asilia (CNG) ili kupata unafuu sasa wametufuata huko,” alisema Jackson Munisi, dereva wa teksi mtandao anayetumia gesi asilia kama mbadala wa mafuta.

Amesema gharama za kubadilisha mfumo kutoka kwenye mafuta kwenda kwenye gesi ni kubwa (kuanzia Sh2 milioni) lakini watu walikuwa wanafunga mkanda wanabadili kwa kujua watapata nafuu.

“Ule unafuu tuliokuwa tunaukimbilia unaanza kupungua, kwa bei ya sasa nilikuwa napata ‘hesabu’ ya bosi nami nabakia na kiasi cha kusogeza maisha, hivyo kitapunguzwa na bei hiyo na hatujui mwaka ujao itakuwaje,” amesema Munisi.

Akizungumzia suala hilo kwa sharti la jina lake kutoandikwa gazetini, mmoja wa viongozi wa kampuni zinazotoa huduma za kubadili mifumo ya magari kutoka kwenye mafuta kwenda gesi, amesema hatua hiyo itaongeza gharama za gesi kwa asilimia zaidi ya 25, hivyo huenda kasi ya watu kukimbilia huko ikapungua.

“Hii huenda ikatengeneza hofu ya watu kuendelea kubadili magari yao kwa kuwa hawajui kama kweli wataendelea kupata nafuu waliyonayo kwa siku zijazo, maana Serikali ni kama imepata chimbo jipya la kodi,” amesema.

Amesema punguzo la kodi kwenye vipuri vya kubadilisha mfumo huo halijaleta matokeo yoyote chanya kwa kuwa lilikutana na changamoto za uhaba wa Dola na gharama kubwa za usafirishaji, hivyo hatua ya kuongeza bei sasa itaumiza.

“Kwa sababu bajeti itajadiliwa kabla ya kupitishwa nafikiri Serikali iangalie upya hatua hii ili watu waendelee kuvutiwa na matumizi ya nishati hiyo kuliko sasa wanavyotaka kuwakimbiza,” amesema.

Related Posts