Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kushirikiana na waandishi wa habari kutoa elimu juu ya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,kupitia mwenyekiti wake Jaji (Rufaa) Jacob Mwambegele, ameeleza kuwa Tume inatambua na kuheshimu mchango wa vyombo vya habari, hasa vya kijamii na kijitali, katika kuwafikia vijana ambao ni walengwa muhimu wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Juni 13, 2024, katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam,katika hotuba yake, Jaji Mwambegele alisema, “Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba vyombo vya habari vikuu bado vinawafikia watu wengi na vina umuhimu mkubwa katika kuwahabarisha na kuelimisha wananchi,” amesema.

Aliongeza kuwa uwepo wa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kwenye mkutano huo utasaidia kueneza taarifa muhimu kwa wadau wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki cha uboreshaji wa daftari.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhani, akiwakilisha mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, alisema kuwa zoezi hilo litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu mwaka 2025. Pia litatoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na ambao wamehama kuhamisha taarifa zao, pamoja na kurekebisha taarifa nyingine kama majina.

“Katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Daftari linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya mwaka 2020 hili ni ongezeko la wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7,” amesema Kailima

Ameongeza kuwa katika zoezi hilo wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa katika Daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.

Amefafanua kuwa siku ya uzinduzi ambayo ni Julai 1 mwaka huu ndiyo siku ambayo pia uboreshaji utaanza katika mkoa wa Kigoma na kuendelea katika mikoa mingine ya Katavi, Rukwa na Tabora. 

“Kwa lengo la kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, uboreshaji utafanyika kwenye mizunguko 13 itakayobainishwa kwenye ratiba. Aidha, zoezi hili litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura,”

“Tunawasihi muendelee kutuunganisha na wadau. Tume itaendelea kuweka milango wazi kwa ajili ya kutoa taarifa za mara kwa mara,” alisema Jaji Mwambegele.

Alifafanua kuwa Tume itakuwa na kituo cha huduma kwa wateja ambacho kitatoa majibu kwa maswali mbalimbali yanayohusiana na uboreshaji wa daftari.

Related Posts