Dar es Salaam. Wadau wamepongeza hatua ya Serikali ya kuondoa ushuru wa forodha kwenye malighafi za kutengeneza taulo za kike, huku wakishauri hatua zichukuliwe kuhakikisha bidhaa hizo zinapatikana kwa gharama nafuu.
Kwa muda mrefu kumekuwapo kilio cha gharama za juu za taulo za kike hali inayosababisha mabinti hususani wanafunzi kushindwa kumudu, hivyo baadhi kutohudhuria masomo wanapokuwa kwenye hedhi.
Edina Lyimo, mwanafunzi wa shule ya sekondari jijini Dar es Salaam amesema: “Mara nyingi ninapokuwa kwenye hedhi huwa siendi shuleni kwa sababu sijisikii huru kutokana na kukosa pedi.”
Akiwasilisha bajeti ya Serikali bungeni jana Juni 13, 2024, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alitangaza kuondolewa kwa ushuru wa forodha katika malighafi zinazotumika kutengeneza bidhaa hizo.
“Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubalia kuendelea kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 au asilimia 25 kwenye malighafi za kutengeneza taulo za kike na taulo za watoto. Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji na kuongeza ajira,” alisema.
Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amesema Serikali imeonyesha kusikia kilio cha wananchi lakini bado kuna hatua nyingi zinazohitajika kuchukuliwa kuhakikisha bei za taulo za kike zinashuka.
“Wazalishaji wengi wa taulo za kike wanatoa malighali nje ya nchi na wanatozwa kodi kubwa kuziingiza, hivyo na wao wanashusha mzigo wa gharama kwa watumiaji. Hatua ya kuondoa ushuru wa forodha itawezesha kupunguza gharama za uzalishaji kwa kiasi fulani,” amesema na kuongeza:
“Hata hivyo, hii haitoshi kufanya bei za pedi zishuke kiasi cha kila msichana kumudu, ili kufikia huko kuna hatua nyingine kadhaa ambazo Serikali inapaswa kuzichukua.”
Gyumi amezitaja kuwa ni kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo hizo ili kuwezesha zipatikane kwa gharama nafuu tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa zinatozwa kodi hiyo.
Hatua nyingine amesema ni Serikali kuondoa utitiri wa kodi inazotoza kwa mnyororo wa uzalishaji ambazo huwalazimisha wazalishaji kuzifidia kwenye gharama ya bidhaa wanazouza.
Eneo lingine aliloshauri kufanyiwa kazi ni Serikali kuanzisha programu zitakazowezesha kupeleka taulo hizo shuleni ili wasichana wapate na isiwe kikwazo kwenye masomo yao.
“Taarifa zinaonyesha wasichana wengi wanaposhindwa kumudu bei ya bidhaa hizi wanatumia vifaa vya kujisitiri ambavyo si salama kwa afya zao,” amesema Gyumi.
Hilo linathibitishwa na msichana kutoka mkoani Arusha aliyeeleza: “Katika jamii yetu kuna wasichana ambao wanatumia kinyesi cha ng’ombe kujihifadhi wakati wa hedhi. Kutokana na ukosefu wa maji wanatumia maziwa ya ngombe kujisafisha au wanatega ule muda ambao ng’ombe anakojoa ili watumie mkojo wake kujisafisha.”
Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben amesema: “Ni hatua ya kupongezwa ila niombe watengenezaji wawe wazalendo ili matokeo ya hiki kilichoamuliwa yaonekane.”
“Tunaweza kusema angalau Serikali imeanza kuona umuhimu wa kulinda utu wa mwanamke, taulo za kike zina nafasi muhimu kwenye maisha ya mwanamke, hivyo hatua kama hizi zinapochukuliwa inaleta matumaini.”