Balozi Ruhinda afariki dunia | Mwananchi

Dar es Salaam. Mmoja wa waasisi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Balozi Ferdinand  Ruhinda (86) amefariki dunia leo Juni 15, 2024 nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam kutokana na maradhi ya kisukari.

Mdogo wa marehemu, Edward Ruhinda amethibitisha kutokea kwa kifo cha kaka yake akisema ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akihudumiwa na madaktari nyumbani kwake hadi umauti ulipomfika.

“Ni kweli amefariki dunia kutokana na maradhi ya kisukari. Amefariki hapa nyumbani kwake akipatiwa huduma na daktari wake,” amesema Edward wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu kifo cha Balozi Ruhinda.

Kuhusu taratibu za mazishi ya Balozi Ruhinda, Edward amesema familia inaendelea na maandalizi hayo na wanatarajia atazikwa Dar es Salaam, Jumatatu Juni 17, 2024.

Balozi Ruhinda alizaliwa Karagwe mkoani Kagera mwaka 1938, ameacha watoto watatu, mke wake pia alishafariki dunia.

Katika uhai wake, Balozi Ruhinda amefanya kazi mbalimbali. Alikuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Canada (1983 – 1988) na China (1989 – 1992). Pia, alikuwa mhariri maarufu wa vyombo vya habari nchini na mmoja wa waasisi wa MCL na Redio Uhuru.

Balozi Ruhinda aliwahi kuwa mhariri mtendaji wa magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo, na yale ya Serikali ya Daily News/Sunday News na Habari Leo kwa nyakati tofauti.

Kwa mujibu wa tovuti ya Serikali yenye taarifa za mabalozi, inaeleza kwamba Balozi Ruhinda alisomea uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kuchukua kozi fupi katika Shirika la Habari la Marekani na China.

Alifanya kazi na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kabla ya kujiunga na Uhuru na baadaye Daily News kama mhariri mtendaji wa wa magazeti ya chama na Serikali mtawalia miaka ya 1970.

Mapema miaka ya 1980, alijiunga na huduma za diplomasia kama Mkurugenzi wa Habari na Utafiti katika Wizara ya Mambo ya Nje.

Baadaye alikuwa ofisa katika ubalozi wa Tanzania nchini Sweden kabla ya kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na baadaye Balozi wa Tanzania nchini China, kabla ya kustaafu utumishi wa umma.

Related Posts