Iringa. Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imemhukumu kifungo cha maisha jela, msafirishaji wa dawa za kulevya, Mwasema Bakari aliyejisalimisha Kituo cha Afya Mtandika.
Mwasema aliyekuwa amemeza kete 58 za heroini zenye uzito wa kilo 1.01 alienda kituoni hapo Machi 31, 2023 akisema amevimbiwa lakini hali yake ilipozidi kuwa mbaya, alieleza amemeza dawa za kulevya.
Kutokana na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri katika mahakama hiyo iliyoketi Iringa, mbele ya Jaji Ilvin Mugeta alimuhukumu kifungo cha maisha jela.
Jaji Mugeta katika hukumu aliyoitoa jana Juni 14, 2024, aliukataa utetezi wa mshitakiwa kwamba Machi 31, 2023 saa 5.00 usiku akiwa eneo la Ruaha Mbuyuni, alitekwa nyara na watu waliompulizia dawa usoni na kumfanya apoteze fahamu.
Alidai kortini alizinduka Aprili 2, 2023 na kujikuta amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa akiwa chini ya ulinzi wa Polisi na kwamba, hafahamu chochote kuhusu kete 58 zilizotolewa kortini kama kielelezo.
Ingawa katika utetezi hakukubali wala kukanusha kuwepo katika Kituo cha Afya cha Mtandika usiku wa Machi 31, 2023 kuamkia Aprili Mosi, alijitetea akiwa Hospitali ya Rufaa Iringa alilazimishwa na polisi kusaini karatasi fulani.
Alivyofika kituo cha afya
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Oleda Kahise anayefanya kazi kituo cha Afya cha Mtandika kilichopo Kilolo, alieleza siku ya tukio saa 6.30 usiku, mshitakiwa alijisalimisha kituoni akidai kuwa na hali mbaya ya kuvimbiwa.
Alimjulisha Dk Genoveva Kavela (Shahidi wa pili wa Jamhuri) wakati anamhudumia aliongea maneno yaliyoashiria amelawitiwa, hivyo akasitisha kumhudumia hadi awe na fomu ya polisi namba tatu (PF3).
Daktari akaamua kuwasiliana na polisi kwa ajili ya msaada na baada ya kuwasiliana na Polisi Kituo cha Ruaha Mbuyuni, walisisitiza mgonjwa huyo kutotibiwa bila kuwa na PF3, hivyo matibabu dhidi yake yakasitishwa.
Ilipofika asubuhi, Oleda Kahise aliyekuwa ofisa tabibu aliondoka na kukabidhi zamu kwa shahidi wa tatu, Veronica Mgandu ambaye ni muuguzi, ambaye wakati akimhudumia mshitakiwa hali yake ilibadilika na kuwa mbaya.
Mshitakiwa akamweleza muuguzi alikuwa na dawa za kulevya tumboni, hivyo naye alitoa taarifa kwa shahidi wa nne wa Jamhuri, Salehe Matinya, mwenyekiti kitongoji cha Mtandika.
Mtandika alim julisha shahidi wa tano, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP), Issa Seleman aliyekuwa mkuu wa upelelezi (RCO) Mkoa wa Iringa aliyefika na makachero wengine na kumchukua mshitakiwa.
SACP na timu yake ambao ni mashahidi wa saba, 10 na 11 walimpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa alikotibiwa na Dk Huruma Mwasipu, aliyekuwa shahidi wa nane, mbele ya shahidi wa tida Brighton Chilale.
Dk Mwasipu katika ushahidi alidai kuanzia Machi 31 hadi Aprili 2, 2023, alitoa kete 58 kutoka tumboni kwa mshitakiwa kupitia njia ya haja kubwa na baada ya kupimwa na shahidi wa sita, Gabriel Jacob, ilibainika ni za heroini.
Mshitakiwa alifikishwa kortini kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya na baada ya kusomewa mashitaka alikana kuyatenda. Alikaa mahabusu kwa kuwa shitaka hilo halina dhamana.
Akichambua ushahidi uliotolewa, Jaji Mugeta alisema unaobishaniwa unaanzia Kituo cha Afya cha Mtandika ambako mashahidi namba 1, 2, 3, 4, 5 na 7 walieleza kukutana na mshitakiwa.
“Mshitakiwa alinishawishi hata kama alikuwepo Kituo cha Afya cha Mtandika, basi alikuwa amepoteza fahamu baada ya kupuliziwa kemikali eneo la Ruaha Mbuyuni usiku wa Machi 31, na kwamba alipata fahamu Aprili 2, akiwa Hospitali ya Rufaa Iringa,” amesema.
Jaji akasema, “Hii hadithi ingawa inawezekana, lakini haiwezekani sana,” akarejea ushahidi wa mashahidi sita wa Jamhuri waliosimulia namna alivyopokewa kituoni hadi kupelekwa Hospitali ya Rufaa Iringa.
“Sina sababu ya kutilia mashaka ushahidi wa mashahidi hao wa Jamhuri ambao haukutikiswa wakati wa maswali ya dodoso. Mshitakiwa hakuwahoji lolote mashahidi walioeleza uwepo wake Kituo cha Afya Mtandika akiwa na fahamu zake,” amesema Jaji.
“Ni msimamo wa sheria kuwa kushindwa kumhoji shahidi katika mambo ya muhimu inapelekea ushahidi wa shahidi huyo kuchukuliwa kuwa ni wa ukweli,” amesema akirejea msimamo wa sheria katika kesi ya Rashid Sarufu dhidi ya Jamhuri.
Amesema hana sababu ya kutilia mashaka ushahidi kuwa kete 58 zilitolewa tumboni kwa mshitakiwa kupitia njia ya haja kubwa kwani ilishuhudiwa na mashahidi wanne na mashahidi namba 8 na 9 ambao ni raia, hivyo ushahidi wao ni huru.
Kutokana na ushahidi huo na vielelezo vilivyopokewa kortini, Jaji Mugeta amesema upande wa mashitaka umethibitisha kesi pasipo kuacha mashaka yoyote na kwa viwango vya kisheria vinavyotakiwa katika kesi ya jinai kama hiyo.
Jaji amesema kusafirisha dawa za kulevya ni kosa linaloangukia katika sheria ya uhujumu uchumi chini ya aya ya 23 sura ya 200 ambapo kifungu cha 60(2) kinatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 20 jela na kifungo kisichozidi miaka 30 jela.
Jaji amesema kifungu hichohicho kinasema pale kunapokuwa na sheria nyingine inayotoa adhabu kubwa zaidi ya kifungu hicho basi mahakama itatoa adhabu hiyo kubwa na kifungu cha 15(1) sura ya 95 kinatoa adhabu ya kifungo cha maisha jela.