Unguja. Wakati kikizinduliwa Kigoda cha taaluma cha Sheikh Abeid Amani Karume katika ukombozi wa maendeleo ya Afrika, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi na marais wastaafu wameeleza umuhimu wa vigoda, wakisisitiza kujikita katika kufanya tafiti.
Kigoda hicho kimezinduliwa leo Juni 15, 2024 na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi, katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza).
Profesa Eginald Mihanjo ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa kigoda hicho.
Marais wastaafu waliohudhuria uzinduzi huo ni Jakaya Kikwete, Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.
Rais Mwinyi akizindua kigoda hicho amesema Mapinduzi ya mwaka 1964, yaliyoleta uhuru wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Zanzibar, hayakuwa tu ya Zanzibar bali yalileta msukumo mkubwa kwa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Amesema baada ya kuunganishwa na Tanganyika Aprili 1964 na kuundwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Karume aliendelea kuwa kiongozi imara katika kujenga Taifa imara na lenye umoja.
Amesema malengo ya kigoda hicho ni kuhifadhi, kuibua na kueneza mawazo na fikra za kiongozi huyo.
Rais Mwinyi amesema pamoja na shughuli nyingine za kigoda, Serikali inashauri kutilia mkazo zaidi masuala ya kufanya tafiti kwa ajili ya maendeleo.
“Kupitia tafiti, mijadala, makongamano, mikutano na machapisho mbalimbali, pomoja na kuendeleza ushirikiano wa ndani na nje ya Afrika ulioanzishwa na Karume baada ya Mapinduzi, sambamba na kuandaa na kutekeleza mipango na kazi za kila siku za kigoda ikiwemo programu za kuelimisha, kufundisha na kuenzi kwa vitendo fikra na falsafa zake kupitia kwenye shule, vyuoni na katika jamii kwa ujumla,” amesema.
Amesema matokeo ya tafiti hizo yatatoa taarifa sahihi kwa watunga sera, hivyo kusaidia kupanga mipango mizuri ya kimaendeleo kitaifa.
Amesema, matokeo ya tafiti husaidia Serikali na wadau wa maendeleo kufahamu changamoto na fursa zilizopo, katika sekta mbalimbali.
“Hivyo nawasihi wanataaluma kutumia fursa ya kufanya tafiti na kazi nyingine za kitaaluma kupitia Kigoda cha Karume ili kustawisha taaluma zenu na kuleta mchango katika jamii zetu,” amesema.
Amesema Serikali kwa upande wake, itafanya kila juhudi za hali na mali kuhakikisha kuwa lengo kuu na malengo mahususi yote ya kigoda yanafanikiwa ili kuleta tija za kihistoria, kitaaluma na za kimaendeleo.
Amezitaka taasisi binafsi na mashirika mengine ya ndani na ya kimataifa, kushirikiana na Serikali katika kukisaidia kigoda kutekeleza majukumu yake.
Walichosema marais wastaafu
Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema kigoda ni kitu cha heshima kinacholenga kuendeleza tafiti na taaluma, akitaja mambo makuu manne ya umuhimu wa vigoda ikiwa ni pamoja na kutoa fursa ya kuunganisha taaluma na mahitaji halisi ya jamii.
Amesema ni uamuzi sahihi kuwa na kigoda kama hicho ambacho kitajikita katika ukombozi na maendeleo ya Afrika.
Pia amesema vigoda hutoa fursa ya kuboresha na kuchochea maendeleo ya fani maalumu na viwango vya elimu katika ngazi ya vyuo vikuu, huku vikitoa fursa ya kukuza ushirikiano na kuimarisha sera ya umataifa wa vyuo vikuu.
Kwa mujibu wa Kikwete, vyuo vingi vinakosa ladha kwa sasa kwa sababu hakuna mchanganyiko wa maprofesa kutoka mataifa mbalimbali kama ilivyokuwa zamni wakati wao wanasoma.
“Maendeleo yoyote duniani yanachangiwa na utafiti, japo utafiti siyo tu unahitaji mipango, lakini unahitaji gharama kwani ndiyo msingi wa maendeleo yake,” amesema.
Ametoa mfano wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere ambacho kilianzishwa mwaka 2008 ambacho kilikuwa cha kwanza kuanzishwa nchini bila kutegemea wafadhili akisema kimeweza kuwakutanisha wanataaluma wengi na kujadili masuala mbalimbali, huku kikizalisha vigoda vingine vinne mpaka sasa.
Alivitaja kuwa ni Kigoda cha Maendeleo ya Nyerere, Kigoda cha Mazingira, Kigoda cha Taaluma ya Kiswahili na Kigoda cha Bioteknolojia, ambavyo vyote vimeonyesha mafanikio makubwa.
“Hivi vigoda vinahimiza kukuza uchumi na kupunguza umasikini, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hiki cha Karume mtazame na maendeleo yake msitazame ukumbozi pekee,” ameshauri.
Amesema kigoda hicho kijadili mambo ya kujenga na malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Shein amesema kigoda kina kazi kubwa kuyatunza Mapinduzi na kuutunza Muungano.
“Haya ni mambo makubwa yanayotakiwa kufanywa na kigoda hiki,” amesema.
Amesema lazima kuyakumbuka Mapinduzi japo wapo wanaonuna lakini ni haki na wajibu kufanya hivyo na kusambaratisha ubaguzi uliopingwa na viongozi hao walioasisi Taifa hilo.
Amesema wapo wanaodhani baada ya Mapinduzi Karume aliendesha nchi kinyume cha sheria lakini jambo hilo siyo kweli, kwani kulikuwa na ‘decree’ ambazo zilikuwa katika maeneo makuu manane zikitoa mwongozo wa kuendesha nchi.
“Karume alikuwa na moyo wa ushajaa, uzalendo, alitangaza elimu bure na viongozi wote waliopo madarakani wamefuata nyayo zake, ikiwa ni pamoja na kuendeleza elimu na afya bure.
Dk Shein amesema lazima ufanyike utafiti, utakaofanywa lazima wakae na kuchambua kwa mustakabali wa Taifa.
Amesema ni vyema kigoda hicho kuzingatia haiba ya Mzee Karume ili kisije kuliwa na mchwa: “Na mchwa wapo, hiki kigoda kinatakiwa kienzi na kufanya yale aliyoyataka Karume, tuwe tayari kukilea kigoda hiki.”
Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume amesema kuanzishwa kwa kigoda hicho lazima viongozi wahakikishe wanasimamia na kuendeleza aliyoyaamini kiongozi huyo.
Amesema lazima waenzi fikra za Mapinduzi kwa kuwaweka watu kuwa wamoja, kupinga ubaguzi wa aina yoyote na kutoa elimu kwa usawa bila kuangalia sura, rangi, mwenye nacho na asiyekuwa nacho.
“Haya ndiyo yalikuwa malengo ya Mapinduzi yaliyoongozwa na Karume na wenzake, kwa hiyo lazima yaendelezwe katika kufanikisha hilo,” amesema.
Amesema hakuna mtu yeyote anaweza kusema ameleta maendeleo katika kisiwa hicho kwani msingi wake uliwekwa na Karume, akitoa mfano wa ujenzi wa majengo ya makazi yaliyojengwa na kiongozi huyo na kuwapatia wananchi bure.
“Maendeleo tunayopata Zanzibar yeye ndio alikuwa mwanzilishi, mtu hawezi kujisifu bali tunaendeleza alipoanzisha,” amesema.
Amesema kuzinduliwa kigoda hicho ni kuandika historia mpya Zanzibar, mawazo na fikra hizo ziwe dira ya maendeleo kwa kuzidisha upendo, uwazi na usawa.
Mwenyekiti wa kigoda hicho, Profesa Mihanjo amesema kwa sasa kuna ukoloni ulioshamiri lakini vijana ambao ndio viongozi wajao hawajui ukoloni kwa hiyo ipo kazi kubwa ya kufanya kama Taifa kuhakikisha kundi hilo linajengwa kwa hamasa ya kujenga mapinduzi ya uchumi.
“Karume alikuwa ni mtu aliyepata PhD bila kuingia darasani, aliona mbali na alikuwa mwenye upeo kwa hiyo nashukuru kwa kuaminiwa kupewa nafasi hii. Tutahakikisha tunaitendea haki ili kumuenzi kiongozi huyu,” amesema.
Mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira amesema Zanzibar ilikuwa imegubikwa na ubaguzi lakini Karume alipigana kuhakikisha anaondoa matabaka.
Kazi zitakazofanywa na kigoda
Makamu Mkuu wa Suza, Profesa Moh’d Makame Haji ametaja kazi za kigoda hicho ni kuendeleza falsafa za ukombozi wa Afrika.
Falsafa ambazo Karume alizisimamia kwa juhudi kubwa wakati wa uhai wake.
Kupitia kigoda, wasomi na watafiti watafanya utafiti kuwakuza wasomi wengine katika falsafa ya ukombozi ili kupata kizazi kipya cha wasomi.
Kigoda pia kitatumika kupanua wigo wa ujuzi na elimu. Kitahifadhi kumbukumbu za kiongozi huyo na harakati zake za ukombozi na maendeleo.
Kuwepo kwa kigoda ni fursa adhimu kuwaunganisha wasomi wa ndani na nje ya Zanzibar, Tanzania na Afrika.