Dar es Salaam. Yanga wikiendi iliyopita ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka ambao ulipitisha matumizi ya bajeti ya msimu uliopita, lakini pia ukapitisha matumizi ya bajeti ya msimu ujao.
Kama ilivyo kawaida ya Yanga kwa miaka ya hivi karibuni mambo yao yamekuwa yakifanyika kwa mpangilio mzuri, mkutano huu ulifana kama mingine ya hivi karibuni.
Ulihudhuriwa na wanachama wao ambao ni viongozi wa matawi zaidi ya 600 lakini pia kulikuwa na viongozi kadhaa wa serikali akiwemo waziri wa Madini Anthony Mavunde, Mama Fatuma Karume, Damas Ndumbaro Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, George Mkuchika Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu pamoja na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa.
Mkutano huu ulifanyika kwenye Ukumbi wa Mkutano wa Mwalimu Nyerere na kuwa na mpangilio mzuri kuanzia mwanzoni hadi mwisho.
Hata hivyo, kumekuwa na baadhi ya maswali ambayo mtaani mashabiki wamekuwa wakihoji na yanaonekana hayakupata majibu sahihi kwenye mkutano ule ulioendeshwa na Rais wa Yanga Hersi Said.
Moja ya swali gumu ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza ni taarifa kuwa Yanga imepata hasara ya zaidi ya bilioni moja.
Kwa mujibu wa taarifa ya Yanga ilionyesha kuwa klabu hiyo iliingiza kiasi cha Sh21.1 bilioni lakini ikatumia Sh22.2 bilioni ambapo ni zaidi ya bilioni moja ya kile ambacho wanachama waliridhia mwaka jana.
Yanga imetumia zaidi ya kile ambacho imekusanya, ikiwa ndiyo timu iliyofanikiwa zaidi kwenye soka hapa Tanzania kwa msimu uliopita.
Timu hiyo ilichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA, lakini ilivuka lengo la mafanikio kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zaidi kuliko wengine wote.
Hii ina maana kuwa Yanga ambayo ilipata Sh2.3 bilioni baada ya kufika robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kama ingemaliza kwenye tegeti yao ya hatua ya makundi basi ingekuwa na hasara ya zaidi kwa kuwa ingekusanya dola 700,000 ambazo ni Sh1.8 bilioni.
Swali ambalo wengi wanajiuliza ni kama Yanga ambayo imetwaa makombe yote msimu huu, ina wadhamini wengi zaidi, ina mashabiki kuliko timu nyingine tena wanaolipa kadi za uanachama ina hasara nani yupo salama kwenye soka nchini?
Inaonekana kuwa timu ambazo zinawania ubingwa na Yanga ambazo hazijachukua ubingwa wowote na hazina mashabiki wengi wanaoingia uwanjani na kulipa viingilio basi zina hasara kubwa zaidi.
Kipengele hiki kimeonekana kuwasumbua mashabiki wa soka nchini na kila mmoja aliyesikiliza ameshindwa kukielewa na kujiuliza ilikuwaje hakikuwekwa kwenye mchanganuo halisi?
Mchanganuo wa matumizi ya Yanga hauna shida unajieleza, lakini tatizo linaonekana kwenye eneo la mapato, Yanga inaonyesha haki ya matangazo iliingiza Sh10 bilioni, mapato ya mlangoni iliingiza Sh1.4 bilioni ada za uanachama ikaingiza Sh613.3 milioni zawadi za ushindi Sh3.4 bilioni.
Huku kote hawana shida wanauliza mapato mengine ya Sh5.4 bilioni ni fedha zilizotoka wapi na mbona ni nyingi?
Hili limekuwa swali kubwa kwa mashabiki ambao wanaamini kuwa kulikuwa na nafasi ya kuwaeleza mashabiki fedha hizo zimetoka wapi.
Lakini wengi wanafikiri pia walikuwa wanatakiwa kufahamu mauzo ya jezi yameingiza shilingi ngapi ili msimu ujao wanunue zaidi kipengele ambacho hakipo kwenye jedwali, labda ndiyo mapato mengine?
Yanga inaonyesha kuwa soka kwa sasa ni ajira ndiyo maana kwenye matumizi yao, mishahara imechukua fedha nyingi zaidi kuliko kitu kingine chochote ambapo imekwenda karibia nusu ya bajeti yao baada ya kutumia Sh7 bilioni.
Hii inaonyesha kuwa ni usahihi kuwa mishahara ya Yanga ni mikubwa kama ambavyo imekuwa ikielezwa.
Ishu nyingine inayoonekana kuchuma fedha zaidi Yanga ni uhamisho wa wachezaji ambapo waliwahamisha kina Pacome Zouazoa na Joseph Guede pamoja na mastaa wengine kwa Sh3.5 bilioni likiwa ndiyo eneo lingine ambalo limeshika nafasi ya pili kwa matumizi ya fedha.
Yanga siyo ya kwanza kupata hasara:
Timu mbalimbali duniani zimekuwa zikipata hasara na hili ni jambo la kawaida kabisa ambapo Manchester United mwaka jana ilipata hasara ya pauni 28 milioni zaidi ya Sh73 bilioni, hivyo kwenye soka hasara ni jambo la kawaida. Msimu uliopita pia Liverpool ilipata hasara ya Sh 9 milioni.
Tunaamini Yanga na klabu nyingine, zinaweza kuepuka hasara hizi, ili ziweze kutumia kile ambacho zinaingiza kama soka linavyotaka kwa kuongeza vitega uchumi vya klabu ili kuvitumia kama sehemu ya mapato, lakini pia kutokana na mapato Yanga inayoingiza inalazimika kuongeza wadhamini kwa kasi, wanachama kulipia kadi zao kila msimu.