KUNDI LA WHATSAPP LA TANZANIA 2015 AND BEYOND LATIMIZA MIAKA 10

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

KUNDI la Mtandao wa Whatsapp la (Tanzania 2015 and Beyond) ambalo lenye wanachama zaidi ya 200 limefanya hafla ya kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. 

Akizungumza na wandishi wa habari leo Juni 15, 2024 Jijini Dar es salaam Mwanzilishi wa kundi hilo Mch.Willence Moshi amesema kundi lao limekutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ya kundi ikiwemo kuboresha mapungufu yaliyopo pamoja na kupokea mawazo mbalimbali.

Mch.Willence amesema kuwa lengo kuu la kundi hilo ni kudumisha undugu pamoja ikiwa ni pamoja na kusaidiana katika katika sherehe na matatizo.

Ameeleza kuwa kundi lao linasimamia misingi ya maadili ambapo watu wenye maneno yasiyofaa huchukuliwa hatua mara moja na kuondolewa kwa muda ili kuimaarisha nidhamu ya wanachama. “Ukiwa mtu mwenye kiburi, ulionywa zaidi ya mara tano tunakuondoa moja kwa moja”Amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Kundi la Tanzania 2015 and Beyond, Bi. Susan Kimambo amesema kundi lao linafuata sheria na taratibu za nchi pamoja na kuongozwa kwa kanuni za kundi ambapo Mwanachama akitumia lugha zisizofaa wanamfanyia uchunguzi wa kimaadili ili kubaini endapo atafaa kuendelea kuwa Mwanachama.

Amesema kuwa miongoni mwa manufaa kwenye kundi hilo ni pamoja na mshikamano ambao umesaidia kudumisha furaha na amani kwa kufungua mwanya wa kusaidiana wakati wa shida na raha.

Bi.Susan amesema kundi hilo limefungua kikundi cha M-KOBA ambapo wanatumia jukwaa hilo kwa ajili ya kufarijiana katika matatizo mbalimbali yanapojitokeza.

Naye, Bw. James Mbowe ambaye ni mwanachama wa kundi hilo amesema katika kundi hilo kuna wanataaluma mbalimbali jambo ambalo limempa fursa ya kuongeza ujuzi ambao unamsaidia katika upande wa kazi yake.

Kundi hilo la Tanzania 2015 and Beyond limejumuisha wanataaluma mbalimbali, wanasiasa, wafanyabiashara pamoja na viongozi wa kidini ambapo limekuwa daraja la mafanikio kwa kutatua changamoto mbalimbali.
















Related Posts