PAMOJA na kutaja kufikia malengo ya kubaki Ligi Kuu, uongozi wa Mashujaa FC umesema msimu ujao hautaki tena presha ya kusubiri mechi za mwisho kukwepa kushuka daraja, huku ukitangaza kuongeza bajeti kutafuta nafasi nne za juu.
Mashujaa ambayo ilishiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza licha ya kumaliza nafasi ya nane kwa pointi 35, lakini ilisubiri michezo mitatu ya mwisho kujihakikishia kuwa salama.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Meja Abdul Tika alisema msimu uliopita waliazimia kubaki Ligi Kuu jambo ambalo walifanikiwa, japokuwa haikuwa kazi nyepesi hadi kusubri dakika za mwisho kujua hatma yao.
Alisema kwa sasa wanahitaji kukamilisha mipango yao mapema ikiwamo usajili na wachezaji kuingia kambini ifikapo Juni 28, ili kumrahisishia Kocha Mkuu kupata muunganiko mapema.
“Tulifanikiwa japo ilikuwa presha kali sana, tunahitaji kufaya usajili mapema ili hadi Juni 28 timu iwe kambini, tuna uhakika tutabaki na benchi letu la ufundi chini ya Abdallah Mohamed ‘Baresi’ alisema Meja huyo.
Tika aliongeza kuwa wakati wakisubiri ripoti ya Baresi Jumatatu ijayo, matarajio yao ni kuongeza bajeti kulinganisha na msimu uliopita kuhakikisha wanawania nafasi nne za juu.
Alisema makosa yaliyoonekana ndani na nje ya uwanja, uongozi utajitahidi kusahihisha na kuboresha ili wanapoenda kuuanza msimu wa 2024/25, Mashujaa iwe tishio kwa timu zote.
“Uongozi utakuwa na tathimini yake, tunafahamu yapo mapungufu huenda yalionekana, tutajitahidi kushirikiana na wadau kuyamaliza na kuboresha penye uhitaji” alisema Kigogo huyo.