NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad
Chande ameipongeza Benki ya Biashara ya Mkombozi,kuwa imepanda kutoka
hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi huku amewasihi watendaji
wa Benki hiyo kutoridhika na hatua waliyofikia, badala yake waendelee
kufanya uhamasishaji ili kuifanya Mkombozi Benki iendelee kukua.
Akizungumza
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande katika Hafla ya Mkombozi Benki
kupandishwa Rasmi kutoka Soko la Ukuzaji Mitaji la DSE (EGM) na kwenda
kwenye Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS) iliyofanyika Kambarage House jijini
Dar es Salaam.
“Hongereni
sana Mkombozi Bank kwa hatua hii mliyofikia, kwa sababu mmepanda hadhi
kutoka hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi sana. Lakini
niwaombe, msiridhike na hatua hiyo mliyoifikia, kwa sababu kuna maneno
yanasema ‘Mpanda patosha, huvuna pa mkwisha.”
“Endeleeni
kuhamasisha ili Bank hii ya Mkombozi iendelee kukua. Kwa hiyo naomba
kutangaza rasmi kwamba Mkombozi Bank imepandishwa rasmi kutoka Soko la
Ujasiriamali (EGM) na kuingizwa Katika Soko Kuu la Uwekezaji (MIMs),”
amesema Naibu Waziri.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, Respige Kimati
amesema kuwa Benki hiyo imewekeza nguvu nyingi ili kuanza kutoa gawio
kwanzia mwakani 2025, kuwa Benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuungana
na Serikali katika kuwashika mkono watu waliopatwa na majanga mbalimbali
ndani ya jamii.
“Tumeshuhudia
ukuaji mkubwa wa faida, ongezeko la amana za wateja, ongezeko la mikopo
iliyotolewa kwa watanzania hasa sekta binafsi, kupanuka kwa mtandao
wetu wa matawi na uwekezaji mzuri katika huduma za benki kwa njia ya
Mtandao, hususani uanzishwaji na usambazaji wa huduma za Benki kwa njia
wa Mawakala”. amesema Kimati
Aidha,
Kimati amesema Malengo ya benki hiyo ni kumkomboa Mtanzania katika
wimbi la umasikini kwa kutoa huduma za kibenki hasa mikopo midogo midogo
kwa watu binafsi wakiwemo vijana na wanawake na mikopo ya kati na
mikubwa kwa makampuni, taasisi za huduma na wafanyabiashara wa kati na
wadogo.
Hivyo, hatua
hii mpya ya kuwa sehemu ya Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS) katika Soko la
Hisa la Dar es Salaam, tunayo imani kubwa kwamba mafanikio zaidi
yanakuja mbele yetu, tunahitaji kuendelea kupata msaada wenu wa dhati na
tunawaomba washirika wetu, wateja wetu, wanahisa, mamlaka mbalimbali za
usimamizi wa sekta ya fedha nchini na watunga sera kuendelea kutuunga
mkono katika safari hii ili Msaada wenu ni muhimu sana katika
kuhakikisha tunatimiza malengo yetu ya muda mrefu na kuboresha huduma
zetu kwa wateja wetu.