Polisi watawanya wananchi kwa mabomu ya machozi

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, limelazimika kutumia mabomu ya machozi, kuwatawanya wananchi waliokuwa wamevamia lori lililokuwa limebeba mafuta ya kula, lililopata ajali, eneo Njoro, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa leo Juni 15, 2024 imesema gari hilo lililokuwa limebeba mafuta ya kula aina ya Korie, lilipata ajali Juni 14, 2024 likitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Arusha.

Kamanda Maigwa amesema katika eneo hilo la ajali, askari mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa na kitu butu kichwani na mwananchi aliyekuwa akipinga amri ya kutawanyika eneo hilo.

Amesema pamoja na jitihada zilizochukuliwa kuwazuia wananchi wasiendelee kupora mafuta hayo, ililazimika polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya katika eneo hilo.

“Baada ya ajali hiyo kutokea, taarifa zilifika kituo cha polisi na askari waliwahi katika eneo la tukio, waliwakuta wananchi wamevamia gari hilo kwa lengo la kupora mafuta hayo na askari mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa na kitu butu  kichwani na mwananchi aliyekuwa akipinga amri ya kutawanyika eneo hilo,” amesema Kamanda Maigwa.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kukimbilia kwenye eneo ambalo ajali imetokea kwa lengo la kufanya uporaji.

“Wananchi wanapozuiwa na askari kuingia kwenye eneo la tukio, wawe wasikivu kwa usalama wao na watambue wakikaidi lazima hatua za kisheria zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kukamatwa,” amesema.

Related Posts