UKISIKIA kunyang’anywa tonge mdomoni ndiko huku, baada ya Raja Casablanca kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Morocco (Batola) uliokuwa unaonekana wazi upo mikononi mwa FAR Rabat inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi.
Nabi na FAR Rabat waliongoza Ligi hiyo kwa muda mrefu kabla ya mambo kutibuka baada ya Raja kuanza kula viporo vyake na jana usiku walimaliza mechi zao kwa msimu huu kwa kutofautiana pointi moja tu, Raja ikimaliza kama mabingwa wakiwa na pointi 72 na FAR ikiwa na 71.
FAR Rabat ilipata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya FUS Rabat, wakati Raja ikishinda ugenini kwa mabao 3-0 dhidi ya vibonde Mouloudia Oujda na kutangaza ubingwa kama utani baada ya kila timu kuchyeza mechi 30.
Hii ni mara ya tatu kwa FAR Rabat ikipoteza dira ya kubeba ubingwa dakika za mwishoni kwani hata misimu miwili hali ilikuwa hivtyo hivyo na taji hilo kwa Raja limekuja baada ya ya mara ya mwisho kutwaa 2019-2020.
Sare na kipigo kimoja ilichopata katika mechi tano za mwisho ndizo zilizomtibulia Nabi kwani Raja yenyewe katika idadi hizo za mechi imeshinda zote ikiwamo hiyo ya jana usiku na kuiduwawa FAR Rabar inayomilikiwa na jeshi la nchini hiyo ambayo sasa litaanza maisha bila ya Nabi anayeenda Afrika Kusini.
Nabi inaelezwa amemalizana na Kaizer Chiefs iliyokuwa ikimsaka tangu msimu uliopita mara alipoachana na Yanga aliyoifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu bara kwa misimu miwili mfululizo.
Timu za Mouloudia Oujda ba Youssoufia Berrechid zikishuka rasmi daraja, huku mabingwa Raja inayobeba taji la 13 ikiifikia Far Rabat, huku Wydad CA ikiwa ndio vinara kwa kutwaa mara nyingi taji hilo (22) tangu ligi ilipoasisiwa mwaka 1957 na kubadilishwa tena kwa mfumo wa sasa kuanzia mwaka 2009.