KIPA wa Yanga, Djigui Diarra imedaiwa ametingisha kiberiti klabuni hapo kwa kuwataka viongozi wa kikosi hicho kumwongezea mshahara zaidi ili aendelee kusalia katika timu hiyo.
Taarifa zilizopo zinadai kipa huyo kutoka Mali, aliyejiunga na Yanga Agosti 8, 2021 akitokea Stade Malien ya nchini kwao, amewaambia mabosi wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho kwa misimu mitatu mfululizo thamani yake kwa sasa imepanda zaidi tofauti na mwanzo jambo linalomfanya kutaka kuboreshewa masilahi.
Kipa huyo ambaye mkataba wake alioongeza mwaka jana unafika mwishoni, amekuwa ndiye nguzo ya Yanga katika kubeba mataji kwa misimu mitatu mfululizo na kuifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
UONGOZI wa Yanga uko kwenye mazungumzo na beki wa kulia wa timu hiyo, Kibwana Shomari ili kuongeza mkataba mpya. Kibwana aliyejiunga na timu hiyo Agosti 9, 2020 akitokea Mtibwa Sugar, amekuwa hana nafasi kikosi cha kwanza kutokana na uwepo wa beki mwenzake, Kouassi Yao ingawa Yanga inataka aendelee kusalia.