Wafanyabiashara Mara walalamikia makato ya benki, watunza fedha nyumbani

Musoma. Baadhi ya wafanyabiashara mkoani Mara wamelalamikia uwepo wa makato makubwa kwenye taasisi za kifedha hasa benki hali inayosababisha baadhi kutokutunza fedha kwenye taasisi hizo.

Madai hayo yametolewa mjini Musoma leo Juni 15, 2024 kwenye kongamano la klabu ya wafanyabiashara wa NMB.

“Kuna makato makubwa, sijui ada, kodi na mengine mengi, kwa hiyo mtu anaona bora tu pesa yake atunze anavyojua kuepuka makato kama hayo,” amesema Adventina Machugu.

“Wakati mwingine wewe unajua una kiasi fulani benki, ukienda kuchukua unakuta kimepungua sana wakati huo tayari umeagiza mzigo, kwa kweli hii inakatisha tamaa, kwanza hakuna uwazi, fedha zinakatwa tu yaani mtu unaona bora tu ujitunzie fedha zako  kwa njia nyingine japokuwa inaweza isiwe salama lakini hakuna namna.”

Katibu wa Chama cha Wafugaji Wilaya ya Butiama, Peter Machugu amezitaka taasisi za fedha kukaa na Serikali kuangalia namna makato hayo yatashuka ili kuwapa nafuu wafanyabiashara na Watanzania kwa jumla.

Amesema kutokana na hali hiyo, wamejikuta wakifanya biashara katika mazingira hatarishi na kulazimika kutembea na fedha kwenda minadani kwa ajili ya kununua mifugo.

“Kama makato yasingekuwa makubwa ina maana tungekuwa tunafanya biashara kwa mtandao tu, unanunua mifugo yako kisha unafanya miamala moja kwa moja, sasa ili kuepuka gharama hizo za ziada, unaamua tu kutembea na pesa zako, tunatamani sana kutumia mifumo ya kibenki lakini tunaona gharama ni kubwa,” amesema Machugu.

Meneja Mwandamizi, Kitengo cha Biashara kutoka NMB Makao Makuu, Reynold Tony amesema hali ya uwekaji wa amana kwenye taasisi za kifedha nchini bado ipo chini na kwamba kutokana na hali hiyo benki yake imekuwa ikibuni huduma mbalimbali ambazo ni rafiki ili kuhakikisha wafanyabiashara wengi wanatumia mfumo huo.

Ingawa hakutoa takwimu lakini amesema wamebaini wapo wafanyabiashara wengi ambao hawatumii mifumo ya kibenki, jambo ambalo sio zuri kwa kuwa utunzaji wa fedha ndani una hatari nyingi ikawamo fedha kuibwa, kuungua moto na mambo mengine mengi.

“Hii hali sio nzuri kwa benki tu hata wafanyabiashara wenyewe, unaweza ukajikuta unapewa mkopo mdogo kuliko uwezo wako kwa sababu miongoni mwa vigezo vinavyotumika kuamua mfanyabiashara apewe mkopo kiasi gani ni mzunguko wake wa biashara ambao unapimwa kwa njia nyingi ikiwamo namna anavyoweka na kutoa fedha benki.

“Lakini pia uwekaji wa fedha benki ukiwa wa hali ya juu ina maana benki itakuwa na fedha za kutosha kiasi kwamba hata riba inaweza kushuka zaidi ingawa sisi riba zetu ni nafuu, hivyo nitoe rai kwa wafanyabiashara kutunza fedha zenu benki kwa kuwa ni salama na faida,” amesema Tony.

Related Posts