‘Wauza unga’ walivyokwaa kisiki kortini

Dar es Salaam. Kweli siku ya kufa nyani miti yote huteleza na hii ni baada ya wafanyabiashara wanne wa Jiji la Dar es Salaam waliohukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya Sh10 bilioni, kukwaa kisiki katika rufaa waliyoikata.

Wafungwa hao, Mirzai Pirbakhshi, Aziz Kizingiti, Said Mrisho na Abdulrahman Lukongo, walihukumiwa adhabu hiyo Desemba 22, 2021 na Jaji Rose Ebrahim wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

Kulingana na ushahidi uliotolewa kortini, wanne hao walikamatwa na polisi Septemba 7, 2011 eneo la Africana, Kinondoni, wakisafirisha kilo 65 za dawa za kulevya aina ya Heroin zenye thamani ya Sh3.3 bilioni.

Katika utetezi wao kortini, walikanusha mashitaka hayo na kuegemea ushahidi wa kutokuwepo eneo la tukio (alibi) na kuiomba mahakama iwaachie huru kwa kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha shitaka na kuacha mashaka.

Wazee washauri wa mahakama walioisaidia mahakama kusikiliza shauri hilo, waliona upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka na kutaka waachiwe huru, lakini Jaji Ebrahim akawatia hatiani na kuwahukumu adhabu hiyo.

Jaji aliwahukumu kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ambayo ni mara tatu ya thamani ya dawa hizo za kulevya, lakini hawakuridhika na kukata rufaa mahakama ya rufani Tanzania, ambayo nayo katika hukumu yake, imeitupa rufaa hiyo.

Katika hukumu yao waliyoitoa Juni 13, 2024 Jijini Dar es Salaam baada ya kuchambua sababu nane za rufaa na majibu ya Jamhuri, jopo la majaji watatu, Barke Sehel, Pantrine Kente, Dk Paul Kihwelo, walisema rufaa hiyo haina mashiko.

Shahidi wa pili wa Jamhuri, Stesheni Sajini Dacto Daniel Dacto, aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio wakati wakifanyia kazi taarifa fiche kutoka kwa msiri wao, huko Africana Mbuyuni, walifanikiwa kuwakamata warufani wakisafirisha dawa hizo.

Kulingana na ushahidi, warufani walikamatwa wakiwa katika magari matatu, Toyota Caldina T107 BAS na Toyota Carina T954 BGT na katika upekuzi, walipata pakti 97 za kulevya ambapo dawa na magari yalipelekwa kituo cha polisi Kurasini.

Upekuzi wa magari hayo ulishuhudiwa na shahidi huru aliyekuwa shahidi wa tatu wa Jamhuri ambaye alielezea hatua kwa hatua namna upekuzi ulivyofanyika na namna vifungashio 97 vya dawa hizo za kulevya vilivyoweza kukamatwa.

Ni kutokana na ushahidi huo na mashahidi wengine, Jaji Ebrahim aliwatia hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela, pamoja na kulipa faini ambayo ni mara tatu ya thamani ya dawa hizo.

Hoja za rufaa zilizokataliwa

Hukumu hiyo haikuwafurahishwa wauza unga hao, wakaamua kukata rufaa mahakama ya rufani wakiegemea sababu sita ambazo hata hivyo baada ya majaji kuzichambua pamoja na kupitia mwenendo wa kesi, waliona hazina mashiko.

Sababu hizo ni pamoja na kuwa maelezo ya kosa katika hati ya mashitaka yalikuwa na dosari kwa kuwa hayakueleza njia iliyotumika kusafirisha dawa hizo na na baadhi ya vielelezo vilipokelewa kinyume cha Sheria ya CPA, marejeo ya 2002.

Mbali na sababu hizo, lakini walieleza kuwa upande wa mashitaka haukuweza kuthibitisha kesi kwa viwango vinavyokubalika kwani shahidi wa kwanza hakuweza kuipa mahakama maelezo ya kisayansi namna alivyothibitisha ni dawa za kulevya.

Hali kadhalika, walieleza kuwa mnyororo wa upokeaji, uhifadhi na uhamishaji vielelezo (Chain of custody) ulikatika na pia Jaji hakuwaeleza kwa ufasaha wazee washauri wa mahakama hoja muhimu za kisheria ili maoni yao yawe na maana.

Related Posts