Zimamoto yabadili upepo ubingwa ZPL

UPEPO umebadilika baada ya Zimamoto kupata ushindi wa tatu mfululizo ndani ya Juni katika Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) na kuipumulia JKU inayoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa muda mrefu, zikitenganishwa kwa pointi moja tu kwa sasa, huku zikisalia mechi za raundi mbili tu kufunga msimu.

Ushindi huo wa juzi uliopatikana kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Ugunja umeifanya Zimamoto sasa kufikisha pointi 61, huku JKU ikiwa na 62 na kila moja ikiwa imecheza mechi 28.

Kabla ya juzi, Zimamoto ilitoka kuzitungua Maendeleo kwa mabao 4-1 na Mafunzo 2-0 mechi zilizochezwa Juni na ushindi wa juzi ulikuwa ni 19 kwa timu hiyo kwa msimu huu ikilingana na JKU iliyokuwa ikihesabu saa tu ili kutangaza ubingwa kabla ya kutibuliwa na Kundemba iliyowalaza 2-0 mechi iliyopita.

Katika mchezo huo wa juzi, Zimamoto ilienda mapumziko ikiwa nyuma kwa kutanguliwa kufungwa na Ngome, baada ya Yusuf Khamis Magomba kufunga bao dakika ya 18.

Hata hivyo, Zimamoto ilirudi kipindi cha pili na moto kwa kusawazisha bao hilo sekundu chache baada ya kuanza kipindi hicho kwa bao la Mahadhi Juma Mahadhi kabla ya Seleman Mgaza kufunga mabao mawili dakika ya 62 na 67 na kumfanya afikishe manane hadi sasa katika ligi hiyo.

Dakika ya 70 Abduhamid Ramadhani Juma alifunga bao la nne kwa Zimamoto na sekunde chache baadae, Ngome ilipata bao la pili la kufutia machozi lililowekwa kiminia na Paulo Godwin Ulomi.

Kipigo hicho kimeifanya Ngome kutanguliza mguu mmoja kuzifuata Maendeleo na Jamhuri kushuka daraja kwani imesaliwa na pointi 27 na kama itashinda mechi mbili za mwisho itafikisha alama 33 ambazo zinaiweka katika nafasi finyu ya kunusurika kushuka daraja, kwani itaombea Kundemba, Hard Rock na New City zipoteze pia mechi za mwisho ili kuwa salama.

Ngome ni kati ya timu nne zilizopanda daraja na kucheza Ligi Kuu kwa msimu huu sambamba na  Maendeleo, New City na Chipukizi ambao ni mabingwa wa Kombe la FA Kanda ya Pemba na mechi yao ya kusaka bingwa wa Zanzibar na atakaoviwakilisha visiwa hivyo katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao ulivunjika dakika ya 98 wakati matokeo yakiwa ni sare ya bao 1-1.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa pia juzi kwenye Uwanja wa Mao B, mjini Unguja Uhamiaji ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 mbele ya Kundemba. 

Bao hilo pekee liliwekwa kimiani na Haji Khamis Haji dakika ya 81 na kuifanya Uhamiaji kufikisha pointi 41 na kuchupa kutoka nafasi ya nane hadi ya sita katika msimamo.

Related Posts