Dar es Salaam. Mmoja wa waasisi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Balozi Ferdinand Ruhinda (86) aliyefariki dunia juzi Juni 14, 2024 jijini Dar es Salaam, anatarajiwa kuzikwa kesho Jumatatu katika makaburi ya Kondo yaliyopo Ununio.
Akizungumza leo Jumapili, Juni 16, 2024 Msemaji wa familia, ambaye ni mdogo wa marehemu, Edward Ruhinda amesema kabla ya maziko, itafanyika ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT), Masaki, saa 6.
Ametaja sababu za Balozi Ruhinda kuzikwa jijini Dar es Salaam, tofauti na utamaduni wao kupelekwa nyumbani kwako, mkoani Kagera kuwa ni kutokana na maagizo aliyoyatoa enzi za uhai wake.
“Balozi Ruhinda alifariki Juni 14, kama familia tumefanya maandalizi ya mazishi yake kama alivyoagiza wakati wa uhai wake. Kwa utamaduni wetu alitakiwa azikwe Karagwe, lakini kwa bahati mbaya mkewe alipofariki alizikwa hapa Dar es Salaam.
“Baada ya tukio hilo, limemfanya atoe uamuzi mgumu kabla hajafariki kwamba hata yeye akifariki itabidi azikwe hapahapa, alipozikwa mkewe,” amesema Edward.
Akielezea ratiba ya mazishi itakavyokua, amesema mwili wa marehemu upo Hospitali ya Taifa Muhimbili:”Kesho asubuhi mwili utaletwa hapa nyumbani kwa muda na familia itaaga kabla haujapelekwa kanisani kwa ajili ya sala saa sita mchana katika kanisa la KKKT Masaki na baadaye makaburini.”
Amesema marehemu ameacha watoto watatu— wa kike wawili na wa kiume mmoja na wajukuu wanne.
Nayo bodi, menejimenti na wafanyakazi wa MCL wazalishaji wa magazeti ya Mwananchoi, MwanaSpoti na The Citizen wameomboleza kifo hicho.
“Balozi Ruhinda atakumbukwa kwa uongozi wake mahiri wa vyombo vya habari, akiwa mtumishi wa Serikali, na kinara wa uwekezaji katika sekta binafsi uliosimika misingi imara iliyochochea mapinduzi makubwa ya weledi na uendeshaji katika sekta ya habari.
“Bila Balozi Ruhinda, MCL isingekuwepo. Tunamuenzi kama mwanzilishi wetu kinara, kwani sisi ni zao la uwekezaji wake binafsi, kwa kushirikiana na wengine,” wameeleza MCL na kuongeza:
“Tunaipa pole sana familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, wanahabari na Watanzania wote kwa ujumla kwa msiba huu mzito. Tunawaombe faraja katika kipindi hiki kigumu.”
Marafiki na ndugu wa karibu na Balozi Ruhinda ambaye pia aliwahi kuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo na yale ya Serikali ya Daily News, Sunday News, wamemwelezea namna walivyomfahamu marehemu na mchango wake katika Taifa la Tanzania.
Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu amemwelezea Balozi Ruhinda kama mwalimu, kiongozi na muongoza njia kwa vijana wengi ambao baadaye walikuja kushika nafasi za juu kiuongozi.
Amesema alimfahamu Balozi Ruhinda miaka mingi, kwani licha ya kuwa mtu wa kwao Karagwe, pia alisoma na mdogo wake wa mwisho.
“Kwa mara ya kwanza yeye aliniajiri kazi magazetini. Nimemkuta akiwa Daily News yeye ni miongoni mwa waandishi na wahariri wazuri sana, Mzee Ruhinda yeye ndiyo gwiji wa uandishi wa habari ana uwezo mkubwa na uwezo wake wa kujua mambo ulikuwa mkubwa sana.
“Licha ya kuwepo katika nafasi alizokuwa nazo akiwa kijana, alihusika sana katika ukombozi wa bara la Afrika wakati huo na rafiki zake walikuwa kina Samora Machele, baadaye akaenda Daily News kama kiongozi wetu akaingia serikalini,” amesema Rweyemamu.
Amesema alikuwa karibu na familia ya Mzee Ruhinda, alijuana naye mwaka 1995 wakati wa kampeni ya Mzee Benjamin Mkapa:”Aliponiomba nimsaidie vitu vidogovidogo na mwaka 2005 nikasaidia pia vitu kidogo ikazidi kutuleta karibu.”
“Baadaye nilifanya naye kazi Bodi ya TBC, nilikuwa makamu mwenyekiti wake kwenye bodi yeye akiwa mwenyekiti hapo nikawa karibu naye sana, alikuwa ananituma huku na kule. Sasa alipokuwa anaumwa miaka 15 sasa nilikuwa nakuja hapa nyumbani, miaka sita na saba iliyopita alikuwa kitandani akitaka jambo nakuja tunazungumza, nachota busara nyingi alikuwa na uwezo mkubwa sana,” amesema.
Salva Rweyemamu, amesema Balozi Ruhinda alienda na mabadiliko kwa kadri teknolojia ya habari ilivyobadilika, kwani alipokuwa mhariri mwaka 1972, wakati huo gazeti ya National list na Standard linazaa Daily News, yeye ndiyo mtu wa kwanza kuingiza vijana wasomi kwenye tasnia.
“Wakati huo kidato cha nne na sita na siyo wale wa chuo kikuu, ndiyo alianzisha wimbi la kuleta vijana wengi kina Profesa Palamagamba Kabudi na vijana wengi… Kangero wengi, yeye ndiyo wa kwanza alifanya mageuzi namna ya kuajiri vijana lile gazeti la Daily News lilipanda kimauzo na likawa linapendwa sana mtaani,” amesema Rweyemamu.
Amesema Balozi Ruhinda ndiye aliyefanya mabadiliko alipokuwa TBC kama miongoni mwa wajumbe waliobadilisha majina kutoka TVT na Redio Tanzania, walivyounganisha Julai mosi, 2007 Rais Mkapa akizindua na ndiye aliyebuni msemo maarufu na kina Tido Mhando ‘Ukweli na uhakika’.
Alipoona ameumwa kwa muda mrefu aliomba kuacha kazi ijapokuwa alikuwa bado anafanya mambo mengi hasa ya kibajeti.
Rweyemamu amesema Mzee Ruhinda alifanya mageuzi mengi makubwa ya kiutawala.
“Alifanya mageuzi mengi kwenye vyombo vya habari na mchango wake yeye ndiyo alianzisha gazeti la Mwananchi na Redio ambayo kwa sasa ndiyo Redio Uhuru. Gazeti la Mwananchi mpaka leo lina heshima kubwa na redio imekuwa kubwa, lakini mwanzo wake ni Mzee Ruhinda,” amesema Rweyemamu.
Rafiki wa karibu na Balozi Ruhinda, Tryphone Rutazamba amesema amekuwa rafiki yake tangu mwaka 1964.
“Yapata miaka 60 sasa nimenufaika mambo mengi kutoka kwake, alikuwa anapenda kutatua matatizo ya watu, lakini zaidi alikuwa anapenda jamii inayomzunguka,” amesema.
Mzee Rutazamba amesema Balozi Ruhinda alifanikiwa katika mengi kwa kupenda kusoma, akisema Ruhinda ni mfano mzuri kwa wanaopenda kusoma, kwani hata nyumba yake imesheheni vitabu vya kisiasa, kidini na vile vyenye kutoa elimu mbalimbali.
“Aliniambukiza kupenda kusoma na kujipatia maarifa kujiendeleza mpaka ukapata maarifa, amekuwa na mchango mkubwa katika jamii, kisiasa, kijamii amefanya kazi Redio Tanzania amejiunga na magazeti ya Uhuru, mchango wake katika jamii hautasahaulika.
“Naweza kumwelezea kwamba alipenda kuishi vizuri na watu, niliona anaishi na kuchangamana na wengi wakisaidiana mambo mengi ya kimaisha, kwa miaka 60 ya urafiki wetu nimejifunza mambo mengi sana,” ameeleza Mzee Rutazamba.
Historia ya Balozi Ruhinda
Balozi Ruhinda alizaliwa Karagwe mkoani Kagera mwaka 1938. Katika uhai wake, alifanya kazi mbalimbali. Alikuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Canada (1983 – 1988) na China (1989 – 1992). Pia, alikuwa mhariri maarufu wa vyombo vya habari nchini na mmoja wa waasisi wa MCL na Redio Uhuru.
Balozi Ruhinda aliwahi kuwa mhariri mtendaji wa magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo, na yale ya Serikali ya Daily News/Sunday News na Habari Leo kwa nyakati tofauti.
Kwa mujibu wa tovuti ya Serikali yenye taarifa za mabalozi, inaeleza kwamba Balozi Ruhinda alisomea uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kuchukua kozi fupi katika Shirika la Habari la Marekani na China.
Alifanya kazi na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kabla ya kujiunga na Uhuru na baadaye Daily News kama mhariri mtendaji wa magazeti ya chama na Serikali mtawalia miaka ya 1970.
Mapema miaka ya 1980, alijiunga na huduma za diplomasia kama Mkurugenzi wa Habari na Utafiti katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Baadaye alikuwa ofisa katika ubalozi wa Tanzania nchini Sweden kabla ya kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na baadaye Balozi wa Tanzania nchini China, kabla ya kustaafu utumishi wa umma.