Dk Tulia awatuliza wakazi wa Mbeya tatizo la maji

Mbeya. Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson amesema tatizo la mgao wa maji litafikia ukomo baada ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira.

Amesema mradi huo  utekelezaji wake umefikia asilimia 18 na unatarajiwa kukamilika Machi mwakani.

Dk Tulia ameyasema hayo leo Jumapili, Juni 16, 2024 baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu kukosekana kwa maji katika stendi ya mabasi ya Nanenane, wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo ya pikipiki 100 kwa Umoja wa Madereva na Makondakta wa mabasi ya Mbeya, Tukuyu na Kyela (Mbetukye).

Amesema Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha changamoto ya maji inakwisha na wananchi wanapata huduma hiyo muhimu bila bugudha.

“Niwahakikishie wana Mbeya, changamoto ya maji lazima iishe. Tulizungumza kuhusu hili kwenye kampeni na sasa mradi wa Mto Kiwira umefikia asilimia 18 ya utekelezaji,” amesema mbunge huyo.

Wakati huohuo, Dk Tulia amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa, akisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo aliyosema inaongozwa na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Pia, amewataka wanufaika wa mikopo ya pikipiki kuwa waaminifu katika urejeshaji wa mikopo ili wengine waweze kunufaika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya, Humphrey Msomba amesema chama kina imani na Serikali katika kuboresha miradi ya maendeleo, ikiwemo ya ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Songwe.

“Miaka 10 tuliishi kwa shida sana na maendeleo yalichelewa haya unayoyafanya Dk Tulia ni kutekeleza ilani ya uchaguzi 2020 kwa kugusa kundi la vijana kujiajiri,” amesema Msomba.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Mohammed Azazi ameshauri vijana walionufaika na mikopo wapate elimu kupitia Chuo cha Ufundi (Veta) ili kupunguza ajali za barabarani.

Naye Katibu wa Umoja wa Madereva na Makondakta, Daniel Jackson ameiomba Serikali kuzungumza na wamiliki wa mabasi kutoa mikataba ya ajira ili kuzuia manyanyaso kwa madereva.

“Idadi kubwa ya madereva wanapitia  manyanyaso kwa  kukosa mikataba ya ajira na wakati mwingine  kutimuliwa kazi pasipo kupata stahiki zao,” amesema.

Wakati huohuo Mbetukye wameiomba Serikali kuingilia kati na iwabane wamiliki wao watoe mikataba ya ajira.

Imeelezwa kukosekana kwa mikataba  ya ajira  kunachangia kukosa haki  za msingi ikiwamo mishahara kwa  madereva na makondakta kufukuzwa kazi bila kufuata utaratibu.

Katibu wa umoja huo, Daniel Jackson amewasilisha ombi hilo kwa mbunge huyo wa Mbeya mjini, Dk Tulia muda mfupi baada ya kuwakabidhi pikipiki 100 zenye thamani ya Sh225 milioni.

Amesema katika umoja huo kuna wanachama zaidi ya 500 ambao ni madereva na makondakta lakini  baadhi yao hawana mikataba.

Kwa upande wake kondakta, Emily Emily wa mabasi ya Tunduma  amesema licha ya kulalamikia hali hiyo mara kwa mara  lakini wamiliki wameziba masikio.

“Licha ya changamoto ya mikataba ya ajira bado hata makubaliano ya fedha za kuwapelekea wamiliki  wa magari hayo ni kubwa pasipo kuangalia hali ya biashara ni vyema mbunge ulivyotupatia pikipiki itakuwa sehemu ya kitega uchumi na kuondokana na ugumu wa maisha,” amesema Emily.

Kufuatia kauli hiyo, Dk Tulia amesema atakutana na wamiliki wa mabasi azungumze nao kwa lengo la kuwekana sawa, kwa sababu yeye pia ni mwanasheria.

Mmoja wa wamiliki ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema suala la mikataba ya ajira kwa kada hiyo hufikiwa muhusika anapoonyesha uaminifu.

Related Posts