Unguja. Wakati Waislamu wakishehereka sikukuu ya Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleimana Abdulla amewataka wazazi na walezi kuwavalisha watoto wao nguo zenye stara wakati wa kusherehekea sikuku hiyo.
Hemed ametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 16, 2024 wakati akizungumza na waumini na wananchi katika msikiti wa Mwembeshauri Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kiongozi huyo amesema ni wajibu kila mzazi kuzingatia mila na maadili ya Kizanzibari kwa kipindi chote cha skukuu na siku nyingine ili kuwaepusha na udhalilishaji kutoka kwa watu wasio na nia njema kwao na Taifa kwa ujumla.
“Ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuhakikisha anamvisha mtoto wake mavazi yanayoendana na maadili ya kizanzibari na kuwa waangalifu kwa watoto wenu wakati mnapowapeleka sehemu za matembezi, hasa katika kipindi hiki cha sikukuu,” amesema Hemed.
Hemed amesema matendo mengi maovu yakiwemo ya udhalilishaji kwa watoto hutokea wakati wa sikukuu, hivyo ni lazima watoto wasimamiwe vyema ili waendelee kuwa salama wakati na baada ya sikukuu.
Kwa mujibu wa Hemed, Serikali inaendelea kupambana na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na kuwataka wananchi kuungana na Serikali katika kupiga vita vitendo hivyo, hasa kwa watoto ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Kadhalika, aliwataka waendelee kutunza na kudumisha amani na utulivu kwa kuwa vitu hivyo vimesaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwa kuwaweka watu pamoja.
Ustadh Ali AbdulRahman amewataka waumini wa dini ya Kiislamu kuhakikisha wanafanya ibada kwa wingi wakitarajia kupata fadhila nyingi kutoka kwa Mungu.