Israel kusitisha mapigano kwa muda kila siku Gaza – DW – 16.06.2024

Vita hivyo vimeingia mwezi wake wa tisa tangu vilipoanza Oktoba 7 mwaka uliyopita.

Kusitishwa kwa mapigano hayo kunakofanyika katika sehemu ndogo tu iliyo kilomita 12 kuelekea mji wa kusini wa Rafah, kumeshindwa kutimiza malengo ya Jumuiya ya Kimataifa na mshirika mkuu wa Israel, Marekani wanaotaka mapigano kusitishwa kikamilifu.

Kulingana na Jeshi la Israel usitishwaji wa mapigano ulioanza saa mbili asubuhi utamalizika saa moja jioni. Hatua hiyo itafanyika kila siku hadi taarifa nyengine itakapotolewa.

Israel Kusini-Israel | Majeshi ya Israel
Vifaru vya jeshi la Israel kusini mwa nchi hiyoPicha: Jim Hollander/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Vita vyasitishwa kwa muda baada ya mazungumzo na Umoja wa Mataifa

Usitishwaji huo wa mapigano unalenga kutoa fursa kwa maloriya misaada kukifikia kivuko cha Kerem Shalom kinachodhibitiwa na Israel, eneo ambalo ndilo njia kuu ya kuingiza misaada.

Kumekuwa na matatizo ya kuingia kwa misaada tangu vikosi vya ardhini vya israel vilipoingia Rafah mwanzoni mwa mwezi Mei.

Jeshi la Israel lilisema usitishwaji huu wa mapigano umekuja baada ya mazungumzo na Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya misaada.

Hatua hiyo ya kusitishwa kwa mapigano lakini ilishutumiwa na wanasiasa wenye misimamo mikali ya kizalendo katika serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wanaopinga kusimamishwa kwa mapigano.

Lakini Jeshi la Israel lilisema mapigano hayasitishwi katika eneo zima la kusini mwa Gaza na pia hakuna mabadiliko katika uingizwaji wa misaada kwa ujumla.

Haya yanafanyika wakati ambapo Israel na Hamas wanatafakari pendekezo jipya la usitishwaji wa mapigano, pendekezo lililowasilishwa na utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden katika hatua kubwa ya kujaribu kufikisha mwisho vita hivyo, iliyochukuliwa na Marekani.

Rais Biden alilielezea pendekezo hilo kama la Israel ila Israel yenyewehaijalikubali na kundi la Hamas limetaka pendekezo hilo lifanyiwe mabadiliko ambayo Israel haiyakubali.

Zaidi ya wanajeshi 300 wa Israel wamefariki dunia

Mapigano yanaendelea wakati Israel Jumapili ikitangaza majina ya jumla ya wanajeshi wake 11 waliofariki katika mashambulizi ya hivi karibuni Gaza, akiwemo mmoja ambaye alifariki katika uvamizi uliofanyika  wiki iliyopita.

Khan Younis Ukanda wa Gaza | Raia wa gaza wakisali sala ya Eid
Raia wa gaza wakisali sala ya Eid Picha: Omar Ashtawy/APA Images/ZUMA Press/picture alliance

Hiyo inaifikisha idadi ya wanajeshi wa Israel waliouwawa tangu Israel ilipoanzisha uvamizi wake wa ardhini wa Gaza kufikia wanajeshi 308.

Utawala wa Israel unasema wanamgambo wa Hamas waliwauwa watu 1,200 katika shambulizi lake la Oktoba 7 na kuwateka wengine 250.

Maafisa katika wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas wanasema zaidi ya Wapalestina 37,000 wameuwawa katika vita hivyo.

Haya yote yanafanyika wakati Waislamu huko Gaza na kwengineko duniani wakiadhimisha sikukuuu ya Eid Al-Adha. Picha kutoka Gaza zimewaonesha waumini wa kiislamu wakisali sala ya Eid mbele ya magofu ya nyumba zao zilizoharibiwa katika mapigano hayo.

Vyanzo: DPA/AP

Related Posts