Mwekezaji wa Simba Mohamed Dewji ‘MO’, amefanya uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa upande anaousimamia, akiwarudisha watu wa mpira ndani ya klabu hiyo.
Akitangaza uamuzi huo usiku huu, MO amesema kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa katika makubaliano na Simba ibara ya 40, amewateua Salim Abdallah ‘Try again’, Mohamed Nassoro, Crescentius Magori, Hussein Kita, Zulfikar Chandoo na Rashid Shangazi.
Wajumbe hao wataingia katika Bodi ya Wakurugenzi ya Simba wakiwa upande wa mwekezaji, ambapo ndani ya majina hayo sura tatu za Magori, Nassoro na Try again ni zile zilizokuwa katika bodi ya kwanza ya klabu hiyo zilizofanikisha Simba kuchukua mataji mara nne mfululizo.
Aidha, MO amesema baada ya mazungumzo ya muda mrefu, amekubali kujiuzulu kwa waliokuwa wajumbe aa bodi hiyo, Hamza Johari na Dk Raphael Chegeni.
“Baada ya kushauriana na Johari kwa muda mrefu, ameniomba apumzike kutokana na kubanwa na majukumu yake ya kikazi, hata hivyo nimemuomba abaki katika Baraza la Ushauri na amekubali,” amesema MO.
“Pia Mwanasimba kindakindaki Raphael Chegeni ameniomba kupumzika kwa kuwa, amekuwa yupo katika bodi mbalimbali naye amekubali kuingia katika Baraza la Ushauri.”