Mradi wa maji kunufaisha wakazi 12,000 Magu

Magu. Wakazi 12,000 wa Kijiji cha Kabila wilayani Magu, Mwanza wataanza kunufaika na mradi wa maji uliotekelezwa na kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) na shirika lisilo la kiserikali la (AFRIcai), ikiwa ni jitihada za kuwapelekea maji safi na salama wananchi wa eneo hilo.

Mradi huo wenye thamani ya Sh215 milioni, unahusisha ufungaji wa pampu ya kuzamisha ndani ya kisima, ujenzi wa nyumba ya pampu, tanki la kuhifadhi maji, mtandao wa mabomba ya maji na vituo vipya vya maji 13 vyenye uwezo wa kutoa mita za ujazo 87,000 za maji kwa mwaka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mrdai huo leo Jumapili Juni 16, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewapongeza SBL na AFRIcai kwa kutoa msaada huo kwa wakazi wa kijiji hicho, huku akisema ushirikiano wao unathibitisha dhamira ya sekta binafsi kwa uwajibikaji wa kijamii na maendeleo endelevu.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi amesema mradi huo unaojulikana kama, ‘Water for Life’ ni miongoni mwa mikakati ambayo kampuni inaiendesha katika mikoa ya Iringa, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mwanza, Singida, Mara, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam, Pwani na Dodoma, ikiwa imewanufaisha zaidi ya watu milioni mbili kwa maji safi na salama.

“Kupitia sera ya Water fo Life hadi sasa tumetekeleza miradi 26 ya maji katika maeneo yenye uhaba wa maji katika sehemu mbalimbali za nchi, ambapo zaidi ya watu milioni mbili wamenufaika na miradi hii inayolenga kutoa maji safi na salama,”amesema Anyalebechi.

Meneja wa Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Rispa Hatibu amesema mradi sio tu utaboresha afya za wakazi wa eneo hilo, bali pia utaongeza tija kiuchumi hususani kwa watoto wa kike na wanawake.

Amesema kundi hilo halitahitaji kutumia saa nyingi kutafuta maji safi na salama sehemu nyingine, huku akibainisha inawapa fursa ya kuhudhuria shule wakiwa huru.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika AFRIcai, Bonus Caesar amesema shirika hilo lina sera zilizojikita katika ustawi wa jamii katika maeneo ya maji, afya, elimu na uwezeshaji. 

“Ushirikiano huu wa kimkakati baina ya SBL na AFRIcai unalenga kuondoa uhaba wa maji kwa kuwapatia maji safi na salama wananchi 11,927 katika vitongoji vya Ilambu, Mlimani, Igogo, Shuleni na Majengo,” amesema.

Naye Doto Khumba mkazi wa Magu, amesema mradi huo ni mkombozi kwa wakazi wa maeneo hayo, hususan wanawake waliokuwa wanatembea umbali mrefu kusaka maji.

“Sasa watapumzika, walikuwa wanapata shida sana na wakati mwingine wanagombana na waume zao kisa maji,” amesema Khumba.

Related Posts