RC Chalamila ampeleka mkewe Simba!

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewaachana mbavu watu kwa vicheko baada ya kuigawa familia yake pande mbili za Yanga na Simba.

RC Chalamila katika kuliweka wazi jambo hilo amesema kwamba kuanzia leo mkewe atakuwa anaishabikia Simba wakati yeye akiendelea kusalia Yanga ambapo kauli yake hiyo iliwafanya watu kuangua kicheko.

Hayo yamejiri katika uzinduzi wa Kitabu cha Yanga uliofanyika jana Jumamosi jijini Dar es Salaam.

RC Chalamila alipopewa nafasi ya kuzungumza katika hafla hiyo, alisema: “Kwa kuwa wenzangu wamezungumza mambo mengi, mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa mamlaka niliyopewa namteua mke wangu kuwa mshangiliaji wa Simba nami kuwa mshangiliaji wa Yanga na uteuzi huu mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu unaanza mara moja,” alisema Chalamila anayefahamika mnazi wa Yanga, aliyeongeza;

“Lakini Naibu Waziri Mkuu niseme tu, ushindi wa Yanga unathibitisha kuwa na dira nzuri, muendelezo bora na umoja walionao, hatuna budi kuwapongeza.”

Yanga ilizindua kitabu hicho kinachofahamika kwa jina la Yanga Yetu Historia Yetu ikiwa ni wiki kadhaa tangu itetee ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho kwa msimu wa tatu mfululizo, huku ikifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupitia miaka 25 tangu ilipofanya mwaka 1998.

Related Posts