Sababu tano zilizoipa Simba ubingwa WPL

Msimu wa 2023/2024 kwa wanawake ulimalizika juzi wakati ambapo Simba Queens ilifanikiwa kutwaa ubingwa bila kupoteza mchezo wowote. Simba ilichukua ubingwa huo wiki moja kabla ligi haijamalizika jijini Mwanza baada ya kuichakaza Alliance Girls kwa mabao 3-0 na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa ajili ya msimu ujao.

Timu hiyo ilibeba ubingwa kwenye mchezo wa raundi ya 16 huku ikiwa imesalia michezo miwili ikifikisha pointi 46 ambazo hazitafikiwa na JKT yenye pointi 43 na Yanga Princess yenye nazo 36, huku juzi ikihitimisha baada ya kufikisha pointi 52 ilipoichapa Geita mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Huu ni ubingwa wa nne wa Simba, ikiwa inashikilia rekodi ya kuwa timu iliyotwaa kombe hilo mara nyingi zaidi, ikifuatiwa na JKT ambao walikuwa mabingwa watetezi wakiwa wametwaa ubingwa mara tatu.

Kuna mambo kadhaa yamechangia Simba Queens itwae ubingwa huu msimu huu na kuzipoteza timu nyingine ikiwemo Yanga ambayo imemaliza nafasi ya ya tatu na JKT ya pili.

Ulinzi mzuri, ushambuliaji moto

Baada ya kupoteza ubingwa msimu uliopita ambao JKT Queens ilibeba, msimu huu ilihakikisha inashinda karibu kila mchezo ili kujiweka sawa.

Mzunguko wa kwanza ambao kila timu inacheza michezo tisa, Simba ilishinda nane na kutoa sare mechi moja dhidi ya Bunda Queens ya mabao 2-2 ugenini.

Tangu raundi ya sita mabingwa hao hawajapoteza mchezo wowote na ikiwa ni miongoni mwa timu zilizoruhusu mabao machache baada ya kufungwa saba pekee msimu mzima.

Mbali na hivyo ndio timu inayoshika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi, ikifunga 55 nyuma ya JKT iliyofunga 59.

Pia msimu huu timu hiyo imefanikiwa kuwachapa wapinzani wao wote, iliichapa JKT nyumbani na ugenini na Yanga nyumbani na ugenini, ikiifunga jumla mabao 6-2.

Benchi la ufundi la kisasa

Msimu uliopita Simba ilifukuza Kocha wake mkuu, Charles Lukula ambaye sababu ya kuondoka ni kushindwa kuipatia timu hiyo ubingwa lakini msimu huu ikiongeza gia baada ya kumchukua mzoefu Juma Mgunda kusaidiana na Mussa Mgosi.

Hawa walisaidiana kuhakikisha timu hiyo inatwaa ubingwa huku Mgosi akiwa ndiye kocha mwenye uzoefu mkubwa zaidi kwenye michuano hiyo kwa sasa. Makocha wote wawili walicheza Simba kwa miaka tofauti lakini pia waliwahi kufundisha timu hizo hivyo kukaa muda mrefu kwenye timu hiyo kuliisaidia kuchukua ubingwa.

Mabingwa hao wa nne wa WPL msimu huu wamesajili wachezaji wanne pekee wawili wa kigeni na wawili wazawa iii kukiongezea nguvu kikosi hicho. Ni timu ambayo imesajili wachezaji wachache ukiachana na JKT waliosajili wachezaji saba na Yanga Princess 13 wachezaji ambao hawakuisaidia.

Kwenye wachezaji wanne wapya, watatu to ndio wameingia kikosi cha kwanza, Riticia Nabbosa kwenye eneo la kiungo, Elizabeth Wambui na Joanitha Ainembabazi eneo la winga. Kitendo cha kuongeza wachezaji hao ambao wana uzoefu na soka hilo kuliisaidia time hiyo kwanza kupunguza bajeti ya usajili na kuliongeza ushindani wa namba kwenye kikosi hicho.

Ukitaja mafanikio ya Simba msimu huu huwezi kuacha kutaja juhudi za wachezaji wazawa ambao wamekuwa na mchango mkubwa.

Eneo la ulinzi Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na Violeth Nickolaus wamekuwa na mchango mkubwa wa kuzuia mashambulizi eneo lao kwani kwenye mechi 18 imeruhusu mabao saba pekee ikiwa sawa na JKT.

Wawili hao wamekuwa na utawala kwenye eneo hilo kitendo kilichompa wakati mgumu wa kupata namba kwa Mkenya Ruth Ingosi ambaye amekuwa akipata dakika chache.

Ukiachana na mabeki, eneo la washambuliaji limekuwa chachu kwenye ligi hiyo ambayo hadi sasa Simba kupitia straika wao, Aisha Mnunka ambayeameibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 20 yamekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo msimu huu.

Sapoti ya mashabiki, viongozi

Kadri ligi inavyozidi kuendelea ndivyo inakuwa na mvuto wa aina yake lakini wanaonegesha hayo ni mashabiki, Simba ndiyo timu pekee kwenye ligi hiyo ambayo ilikuwa na mashabiki wengi zaidi msimu huu na misimu miwili iliyopita.

Mashabiki wa Simba wamekuwa wakisafiri na timu hiyo na mfano mzuri ni mchezo dhidi ya Alliance ambao walisafiri na Coaster kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kufunga mkono timu hiyo.

Lakini pia timu hii inaweza kuwa ndiyo yenye sapoti kubwa zaidi ya viongozi wa juu wa timu hiyo, ni rahisi mara kwa mara kumuona Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Iman Kajula jukwaani, Ahmed Ally na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Asha Baraka ambaye ndiye msimamizi wa timu hii.

Straika wa timu hiyo, Aisha Mnunka ambaye ameibuka mfungaji born anasema suala la kuchukua ubingwa limewaongezea kujiamini zaidi baada ya msimu uliopita kupoteza.

“Kama tungepoteza msimu huu tungeumia sana kwa sababu msimu uliopita tulipoteza mechi za mwisho hivyo tumefurahi kuchukua Ngao na kombe hili la ligi tunaomba mashabiki waendelee kutuunga mkono,” alisema mshambuliaji huyo.

Kipa wa Simba, Carolyne Rufa ambaye ameanza kwenye michezo yote ya timu hiyo alisema ni jambo zuri kuona wanatwaa ubingwa huu kwa kuwa msimu ulipita walioumia sana kuupoteza.

“Nafurahia kuchukua ubingwa japo msimu uliopita niliumia kutokana na kupoteza kwa pointi moja, kitendo cha mashabiki kuja kuisapoti timu ya kike ni jambo kubwa na ubingwa sio wetu pekee ni wao pia.”

Makombe Ligi Kuu Wanawake

2016/17 – Mlandizi Queens

Related Posts