ACHANA na michuano ya Euro 2024 inayoendelea huko Ujerumani, unaambiwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora kuna bonge la mechi la kuamua timu ya 16 ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Wenyeji Tabora United iliyofumuliwa bao 1-0 ugenini na Biashara United ya Mara itakuwa na dakika 90 za kuamua kama iendelee kucheza Ligi Kuu kwa msimu wa pili au irudi Ligi ya Championship iliyoikacha msimu uliopita ilipopanda daraja ikitumia jina la Kitayosce ikiwa sambamba na JKT Tanzania na Mashujaa.
Kuanzia saa 10:00 jioni timu hizo mbili zitarudiana na mshindi wa jumla ataungana na klabu 15 zilizojiahakikisha kukinukisha Ligi Kuu ijayo zikiwamo Pamba Jiji na KenGold zilizopanda mapema kutoka Championship, sambamba na klabu 13 zilizosalia katika ligi hiyo iliyomalizika hivi karibuni.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Karume, Musoma, Biashara ilitumia dakika za nyongeza kupata ushindi kwa njia ya penalti ya dakika ya 99 iliyofungwa na Herbert Lukindo katika mchezo uliovurugwa na maamuzi ya kustaajabisha ya waamuzi alioikubali penalti hiyo baada ya awali kuashiriki kwamba ni kona, huku Tabora ikicheza pungufu baada ya Andy Bikoko kupewa kadi nyekundu.
Makocha wa timu zote wametambuiana juu ya mechi hiyo, kila mmoja akijinasibu wamejiandaa kushinda ili waicheze Ligi Kuu ijayo.
Kocha wa Biashara, Amani Josiah, alisema baada ya ushindi wa nyumbani wa bao 1-0, leo wataingia Ali Hassan Mwinyi kwa nia ya kulinda ushindi huo ipande daraja, kwani ndoto za kupanda moja kwa moja zilishakwama mbele ya Pamba na KenGold.
“Tumejiandaa vya kutosha na wachezaji wanajua umuhimu wa mchezo huu wa ugenini, tunaamini Tabora itatuwekea ngumu ikiwa nyumbani, lakini tumeshajipanga kuona tunamaliza mpango tuliouanza katika mechi ya kwanza,” alisema Josiah.
Ofisa Habari wa Tabora, Christina Mwagala, alisema benchi limejiandaa kuwaondolea machungu mashabiki baada ya kupoteza ugenini na kukiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 4-0 mechi iliyopita za play-off dhidi ya JKT Tanzania iliyosalia ligi kuu.
“Tunawaambia mashabiki timu imeandaliwa kupindua meza, mechi haijaisha hadi tumalize dakika 90 za nyumbani , hivyo wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono na wachezaji wamepania kuwapa faraja kwa kuibakisha timu katika Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao,” alisema Mwagala aliyewahi kuwa kuwa Ofisa Habari wa KMC kabla ya kutua kwa Nyuki.