TPA yaeleza mchanganuo wa gawio ililolitoa Serikalini

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imesema kiwango cha gawio ililolitoa katika mwaka wa fedha 2018/19 kiasi cha Sh480 bilioni kilihusisha bakaa ya magawio ya miaka kitano ya fedha iliyopita.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema Sh153.9 bilioni iliyoitoa kama gawio kwa Serikali imetokana na asilimia 15 ya mapato yake ghafi ya robo tatu kati ya nne za mwaka 2023/24.

Kwa mujibu wa TPA, katika robo tatu ya mwaka  ambayo ni sawa na miezi tisa, mamlaka hiyo imekusanya jumla ya Sh1.038 trilioni.

Kutokana na mapato hayo kwa mujibu wa sheria, mamlaka hiyo ilipaswa kutoa gawio la Sh155.7 bilioni na fedha iliyobaki yaani Sh1.78 bilioni itaitoa kabla ya kufungwa kwa mwaka huu wa fedha.

Mchanganuo wa kiwango hicho cha gawio la TPA, umetokana na kuibuka kwa kile ambacho mamlaka hiyo imekiita upotoshaji juu ya kiwango ilichokitoa kudaiwa kidogo zaidi ya kilichowahi kutolewa mwaka 2018/19 cha Sh480 bilioni.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kupitia taarifa kwa umma aliyoitoa leo Jumapili, Juni 16, 2024, amesema gawio hilo lilihusisha bakaa ya magawio ya miaka mitano ya nyuma kuanzia 2013/14 hadi 2017/18.

Bakaa hiyo, amesema ilikuwa Sh338.7 bilioni akifafanua:”Hivyo gawio la Sh480 bilioni lililotokewa mwaka 2018/19 halikutokana na asilimia 15 ya mapato ghafi ya mwaka huo kama ilivyosemwa katika taarifa hiyo.”

Badala yake, amesema gawio halisi la mwaka huo wa fedha lilikuwa Sh141.3 bilioni, ambalo ni asilimia 15 ya jumla ya mapato ya Sh938 bilioni yaliyokusanywa mwaka 2018/19.

Related Posts