Dar es Salaam. Wajasiriamali wanaofanya shughuli zao kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli jijini hapa wameeleza wamiliki wa mabasi kutoshusha na kupakia abiria katika kituo hicho kunavyosababisha biashara zao kudorora.
Wasema biashara zao zinategemea wateja ambao ni abiria, kutokana na mabasi kutoingia kituoni hapo wanakosa wateja na mapato yao yanashuka, hivyo kuiomba Halmashauri ya Ubungo kuinusuru kuweka sheria itakayolazimisha mabasi yote yaanzie katika kituo hicho.
Katika kituo hicho kwa sasa yanaingia mabasi 200 pekee kwa siku kati ya 420 yaliyokuwa yanatakiwa kushusha na kupakia.
Hata hivyo, Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo amesema hakuna hujuma inayofanyika isipokuwa wao wanajua wanaoshusha na kupakia ndani au nje ya stendi hiyo wote wanazingatia sheria za nchi.
“Tunaamini wote wanafuata sheria kwa sababu mtu hawezi kwenda kuwekeza nje kwa kujenga hadi ofisi useme hajafuata sheria. Lazima ufuate sheria na taratibu zote,” amesema.
Mwalongo amesema wote wanaoegesha magari na kushusha nje wanafuata sheria na kama wasingekuwa wanafuata sheria wasingepata leseni za biashara hiyo.
Wakati akieleza hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Aron Kagurumjuli amesema tayari wameanzisha msako maalumu wa kukamata mabasi ambayo hayashushi na kuanzia safari zake katika kituo hicho.
“Jana tumeanza msako huo wa kukamata mabasi yanayoshindwa kuzingatia utaratibu huo na wanatozwa faini kulingana na sheria inayoelekeza. Ujumbe wangu ili wasikutane na adhabu ni lazima mabasi yazingatie utaratibu huo,” amesema.
Mwananchi Digital imezungumza na mmoja wa kiongozi kutoka kituo hicho ambaye ameomba hifadhi ya jina lake amesema jumla ya mabasi saba yameshakamatwa siku ya leo, na kila moja limepigwa faini ya Sh1 milioni.
Wakizungumza Dar es Salaam leo Jumapili, Juni 16, 2024 wajasiriamali hao wamesema kinachoendelea kwa wamiliki wa mabasi kugomea kushusha mabasi yao katika kituo hicho ni hujuma, hivyo lazima kuwekwe utaratibu wa kuwataka kutimiza takwa hilo.
Uhuru Kitima, Mjasiriamali wa eneo hilo amesema kinachoendelea katika kituo hicho kilichojengwa kwa gharama kubwa hakikubaliki hivyo halmashauri ichukue hatua kurejesha heshima yake.
“Kituo kinakuwa gofu wateja hakuna mabasi hayapiti hapa watu biashara hazifanyiki tofauti na tulivyoahidiwa mwanzo wakati tunaamishwa kutoka stendi ya Ubungo kuja hapa Mbezi kuwa fursa zitafunguka,”amesema.
Kitima amesema anafanya biashara ya chakula kwa sasa anapata hasara wateja hapati na mauzo yamepungua kwa asilimia kubwa wakati zamani kwa siku alikuwa anapata zaidi ya Sh70,000 lakini kwa sasa Sh25,000 na ana wafanyakazi.
“Biashara zetu zinategemea watu sasa watu hakuna mambo hayaendi,”amesema.
Naye,Maulid Ramadhan amesema ili heshima ipatikane kwa stendi hiyo ya mikoani lazima abiria washuke kwenye kituo hicho ili wakaguliwe kwa kuwa ina kila kitu ikiwemo idara mbalimbali za kiusalama.
Amesema wilaya hiyo inategemea kupandisha mapato kupitia stendi hiyo lakini ongezeko la vituo holela kunaikosesha dhamira ya Serikali kufikia malengo yake.
Naye, Laura Ngarama amesema stendi hiyo imetumia fedha nyingi kujengwa hivyo Serikali iangalie kwa kina wale wanaogoma kushusha abiria ndani.