Unguja. Watumishi wa Mapato Zanzibar (ZRA) wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuepuka rushwa katika kazi zao za ukusanyaji wa mapato.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ZRA, Profesa Hamed Rashid Hikmany, ametoa kauli hiyo Juni 16, 2024 kwenye semina maalumu ya watumishi wa mamlaka hiyo kuhusu maadili kwa watumishi wa umma na kupambana na rushwa.
Amesema watumishi hao hawapaswi kupokea rushwa kutoka kwa walipakodi ili wawasaidie wafanyabiashara kukwepa kodi na kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa nchini.
Amewataka wafanye kazi kwa uadilifu ili waweze kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali. Katika mwaka wa fedha 2024/25 ZRA imepangiwa kukusanya zaidi ya Sh800 bilioni.
“Lazima tuzingatie uadilifu wa kazi zetu, mtumishi wa ZRA kumsaidia mlipakodi kukwepa kodi ni kosa kubwa na Serikali itapoteza malengo yake. Kwa hiyo hili tulizingatie katika utendaji kazi wetu,” alisema Profesa Hikmany
Kamishna Mkuu wa ZRA, Yusuph Juma Mwenda amesema ZRA inafanya semina mbalimbali kwa watumishi wake ili kuwakumbusha watumishi hao wajibu wa kuzingatia maadili katika ukusanyaji wa mapato.
“Tutaendelea kufanya semina endelevu kwa ajili ya kujenga uwezo kwa watumishi wote wa ZRA, ili kuwakumbusha kwamba wana wajibu gani katika kutimiza maadili na hatimaye kufanya kazi kwa weledi,” alisema Kamishna Mwenda.
Kwa mujibu wa Mwenda, semina wanazopatiwa watumishi wa ZRA zina msaada mkubwa katika kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari, hivyo anewataka kuzingatia huduma bora kwa wateja pale wanapokuwa kwa walipakodi wakitekeleza majukumu yao.
Akizungumza kuhusu kutenda haki kwa walipakodi, Mwenda amewataka watumishi wa ZRA kuhakikisha kunakuwa na usawa katika ulipaji wa kodi na kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
“Wekeni usawa kwa walipakodi, kuwaonea ni ukosefu wa maadili,” alisema Kamishna Mwenda.
Hata hivyo, aliwapongeza watumishi wa ZRA kwa kazi nzuri wanayoifanya katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwani kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni mamlaka hiyo imepata mafanikio makubwa.
Kwa kipindi cha miezi 11 kuanzia Julai 2023 hadi Mei 2024, ZRA imekusanya Sh666 bilioni.
Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi wa kodi na maadili ya wafanyakazi ZRA, Uwesu Uwesu amesema kuwapatia watumishi semina kama hizo kunasaidia kuwakumbusha maadili, kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na rushwa kwa kuwa mafunzo hayo ni chachu katika utendaji kazi wao.
Watumishi 131 wa ZRA wamenufaika na semina hiyo ya maadili na kupambana na rushwa kwenye utekelzaji wa majukumu yao.