WCF yatoa elimu kwa vyombo vya habari kuhusu fidia kwa wafanyakazi

Vyombo vya habari nchini vimehimizwa kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika kutoa elimu na habari sahihi kwa umma kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma wakati wa kikao kazi kati ya Mfuko huo na Wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika mjini Kibaha Pwani ambacho kiliratibiwa na WCF kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania.

Dkt. Mduma alisema WCF ina jukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi hapa nchini ikiwa ni pamoja na umuhimu wa waajiri kujisajili na kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao katika Mfuko huo na wanategemea vyombo vya habari katika kutimiza jukumu hilo.

“Ushirikiano kati ya WCF na Jukwaa la wahariri na vyombo vya habari kwa ujumla ni muhimu sana katika kuhakikisha umma wa watanzania unapata elimu na habari sahihi kuhusu huduma tunazotoa. Na sisi WCF tutaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kwa kuwa tunaamini ndio njia kuu ya kutufikishia habari zetu kwa umma,” alisema Dkt. Mduma.

Dkt. Mduma pia aliwahakikishia wahariri hao kuwa hali ya Mfuko huo ni himilivu kutokana na kufanya uwekezaji katika maeneo na sekta ambazo ni salama na za kuaminika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Bw. Deodatius Balile alieleza kuridhishwa na ushirikiano uliopo kati ya WCF na tasnia ya habari nchini katika jukumu la kuhabarisha umma na kuushauri WCF kuweka mikakati kuhakikisha unakuwa endelevu na stahimilivu kwa kuwa ni mkombozi wa wafanyakazi wanaopata madhila mbalimbali wakiwa wanatakeleza majukumu yao ya kila siku.

“Tunajivunia kufanyaka kazi na WCF na tutaendelea kushirikiana na kuhimizana juu ya umuhimu wa waajiri kujisajili na kuwasilisha michango ya wafanyakazi wetu katika mfuko huu. Nawaomba tu muendelee kutenga bajeti maalum itakayoviwezesha vyombo vya habari kufikisha elimu hii ya fidia kwa wafanyakazi,” alisema Bw. Balile.


Jumla ya wahariri 20 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini walihudhuria kikao kazi hicho.

Related Posts