Abdallah Shaibu ‘Ninja’ agoma kurudi DR Congo

JAPOKUWA dirisha la usajili halijafunguliwa rasmi, lakini timu zinaendelea kuimarisha vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao, hivyo haitakuwa ajabu kusikia mchezaji anatoka sehemu moja kwenda nyingine.

Hivi karibuni, Mwanaspoti limefanya mahojiano na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’, baada ya kuvunja mkataba na iliyokuwa klabu yake ya Lubumbashi Sport ya DR Congo na huenda msimu ujao akaonekana na timu mojawapo za hapa nchini.

Ipo hivi, Ninja alisaini mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo na baada ya kuutumikia mmoja, akavunja uliobakia na sasa anaangalia maisha  mapya kwenye timu nyingine inaweza ikawa Tanzania au nje.

Timu zinazotajwa kuhusishwa na beki huyo ni Singida FG, TP Mazembe na FC Lupopo na mambo yakienda sawa mojawapo anaweza akasaini.

Ninja anabainisha: “Ni kweli kuna timu hapa Tanzania nimeanza nayo mazungumzo, ila ni mapema sana kuitaja, ila kwa DR Congo ni TP Mazembe, FC Lupopo na AS Vita,” anasema.

HUMWAMBII KITU KUHUSU FEI

Kama kuna kitu alikuwa anatamani kuona kikitokea ni kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ (mabao 19) anachukua kiatu cha ufungaji bora, lakini bahati haikuwa yake baada ya Aziz Ki wa Yanga aliyemaliza na mabao 21 kukitwaa msimu ulioisha.

“Kati ya viungo bora Tanzania, huwezi kuliacha jina la Fei Toto, wakati wanashindana na Aziz Ki kufunga, nilikuwa nampigia simu, awe anaamka kusali usiku, ili Mungu amsaidie, alikuwa akifanya hivyo anafunga.

Anaongeza: “Kuna wakati mwingine huwa naona anavyoandamwa na mashabiki, huwa namshauri achukulie kama chachu ya kujituma kwa bidii, ipo siku hali hiyo itaisha, kwani aliondoka Yanga ikiwa bado huduma yake ikiwa inahitajika, hivyo siyo jambo jepesi kushangiliwa, kwangu naichukulia ni ishara ya upendo wa watu wa Yanga kumpenda Fei.”

Pamoja na hilo, anakiri Aziz Ki ni mchezaji aliye na ujuzi mkubwa na alistahili kukinyakua kiatu cha dhahabu.

Ukimuuliza analizungumziaje tukio la Fei Toto kutokuwapo wakati wenzake wanavikwa medali za Kombe la Shirikisho (FA) kwenye ardhi ya nyumbani Zanzibar, atakujibu: “Huwezi kujua alipatwa na kitu gani, Fei ni binadamu, kama kuna vitu sivipendi ni kumhukumu mtu kabla ya kumuuliza, sikumuuliza hilo na wala sikuona.”

UTOFAUTI WA LIGI YA TZ NA CONGO

Anasema japokuwa ushindani wa uwanjani ni uleule, ila ligi ya Tanzania ni bora zaidi, kutokana na kuzingatia ratiba za mechi pia inaonyeshwa kwenye luninga, jambo linalowafanya wachezaji iwe rahisi kuonekana sehemu mbalimbali.

“DR Congo mnaweza mkafika uwanjani, halafu mnaambiwa leo hakuna  mechi, kwao hilo ni jambo la kawaida, nadhani ni kutokana na amani kuwa ndogo na ikumbukwe ilikuwa kipindi cha uchaguzi.”

Anaongeza: ”Tanzania mechi zinaonyeshwa, ila DR Congo zinaonyeshwa zile muhimu tu, mfano zile za kusaka bingwa wa nchi, nje na hapo huwezi kujua kinachoendelea kwa mchezaji aliyepo katika nchi hiyo, hata kama anafanya vizuri, ngumu hata kuitwa timu ya taifa.

“Timu za Tanzania, zina kawaida ya kuwatangaza wachezaji wao kupitia mitandao yake ya kijamii, DR Congo wanatumia zaidi Facebook, pia hawana mwamko wa kuandika vitu wanavyofanya wachezaji, kusema kweli Tanzania tupo mbali sana.”

Anayazungumzia  maisha ya DR Congo kwamba ni magumu hasa kwa mgeni, kwani hakuna uhuru wa kutembea, kila mtaa, kwenye daladala ni jambo la kawaida kukutana na askari walioshika silaha, jambo linaloleta wasiwasi.

“Wakati nafika DR Congo niliambiwa kabisa mwisho wa kutembea ni saa 3:00 usiku, ukivuka muda huo askari akikukamata lazima utampa pesa ama kupata matatizo, sasa kule kuna sehemu ya Watanzania ambako chakula cha nyumbani kinapatikana, pia wanaonyesha mpira ukichelewa tu, basi ujue unakumbana na balaa,” anasema.

Msimu ulioisha kwake ulikuwa wa aina gani?

”Wakati najiunga na Lubumbashi, nilitoka kuwa majeruhi, kwani nikiwa Yanga niliumia msimu wa 2021/22 na baada ya kupona, sikuwa napata nafasi, kitendo cha kucheza DR Congo, kimefanya niwe fiti na kujiamini, hivyo ulikuwa msimu mzuri kwangu.”

“Kama mliona picha niliyopiga na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alinipigia simu niende kwenye mechi ya FC Lupopo na Maniema, nilipofika getini nataka kuingia kama mchezaji, nilipigwa na askari, unaweza ukaona ni kiasi gani usalama ni mdogo, kuhusu mabomu ndio usiseme,” anasema.

Ukimuuliza alizungumzia kitu gani na Injinia Hersi, atakwambia: “Alinishauri nijaribu kuangalia nchi nyingine ya kucheza ama kurejea Tanzania kujipanga upya, aliona uhalisia ulivyo, pia alishuhudia mechi niliyocheza dhidi ya TP Mazembe, alisema umeonyesha kiwango kikubwa, lakini ngumu kuonekana.

Anaongeza: “Nimejifunza jambo kuhusu Injinia, anasajili wachezaji wazuri, kwa sababu anakwenda mwenyewe viwanjani, mfano ligi ya DR Congo haionyeshwi, ila alikwenda kufuatilia wachezaji.”

Ninja pia anamuelezea beki wa kushoto Chadrack Boka. Anasema: “Ni beki mzuri. Kama ni kweli anaenda Yanga, basi watakuwa wamepata mchezaji mwenye ubora unaoendana na wao.”

Anasema Yanga, imejijengea misingi ya kuendeleza ubora kila msimu, anaona ulioisha ilikuwa hatari zaidi, hivyo ilistahili kunyakua mataji muhimu.

“Naona kila msimu Yanga, inaimarika hilo siyo bahati mbaya, imejipanga, unaona aina ya usajili wao, ukiangalia safu yao ya ulinzi naiona ilikuwa ndiyo the best ukilinganisha na timu zote za Ligi Kuu,” anasema.

Kuhusu Simba, anasema inapaswa kujipanga kusajili wachezaji wazuri na aliyemuona amefanya vizuri ni Said Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyekuwa kinara wa mabao 11 ndani ya kikosi hicho.

Ukiachana na hilo, anasema wakati yupo Yanga, wachezaji ambao alikuwa anajipanga kuwakaba ni Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco.” Mfano Okwi tulikuwa tunataniana kwamba unatakiwa kwenda kumkaba kwa udhu, kwa maana ukimkamia unaweza ukasababisha kadi nyingi.”

Ninja alisaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, lakini aliamua kuvunja mkataba wa mwaka mmoja ambao ulisalia na anataja sababu ya kufanya hivyo.

“Asilimia kubwa ya timu za DR Congo ni za viongozi wa serikali, Rais wa Lubumbashi alikuwa anagombea ugavana, baada ya kukosa nafasi hiyo, hakuwa karibu na timu ikawa inapitia wakati mgumu, ikawa shida.” 

Related Posts