Afisa wa juu wa wizara ya elimu nchini Ujerumani amefutwa kazi baada ya kushughulikia vibaya mzozo kuhusu uhuru wa masomo na haki ya kuandamana.
Sabine Döring ametuhumiwa kutaka kukiwekea vikwazo, pamoja na kupunguzwa kwa fedha zinazotolewa kwa wahadhiri wa vyuo vikuu ambao walizungumza dhidi ya kuondolewa kwa kambi ya waandamanaji wanaounga mkono Wapalestina katika chuo kikuu cha Berlin.
Ilifichuliwa Jumapili kuwa Waziri wa Elimu wa Ujerumani Bettina Stark-Watzinger alituma ombi kwa Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani kumfuta kazi Döring.
Soma pia: Polisi yaondoa waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina chuo kikuu cha Berlin
Ombi hilo lilifuatia ripoti ya shirika la utangazaji la Ujerumani ARD kuhusu barua pepe ambayo ilionyesha kwamba ukaguzi wa kisheria ulikuwa umeanzishwa ndani ya wizara ili kujua iwapo ufadhili wa wasomi hao unaweza kukatwa.
Ukaguzi huo ulianzishwa na Döring, ambaye anahusika na vyuo vikuu. Döring ni afisa wa pili wa cheo cha juu katika wizara na, tofauti na Stark-Watzinger, siyi afisa wa kuchaguliwa bali mtumishi wa umma.
“Nimepanga ukweli wa kesi hiyo kuchunguzwa kwa kina na kwa uwazi,” alisema Stark-Watzinger. Alithibitisha kwamba “uchunguzi wa matokeo yanayoweza kutokea kulingana na sheria ya ufadhili kwa hakika uliombwa kutoka idara husika.”
Döring alikiri kwamba “ilionekana kuwa alijieleza kwa njia ya kupotosha wakati wa kuagiza ukaguzi wa kisheria,” Stark-Watzinger alisema.
“Hata hivyo, hisia ilijengeka kuwa Wizara ya Elimu ilikuwa inazingatia kuchunguza matokeo chini ya sheria ya ufadhili kwa msingi wa barua ya wazi iliyofunikwa na uhuru wa kujieleza,” aliongeza waziri huyo.
Kwa nini wasomi walilengwa?
Wanafunzi wapatao 150 wanaounga mkono Wapalestina, wakipinga mashambulizi ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza, waliweka kambi katika Chuo Kikuu Huria cha Berlin mapema mwezi Mei. Chuo hicho kiliita haraka polisi, ambao walisafisha eneo hilo.
Kufuatia hatua hiyo, wasomi 100 kutoka vyuo vikuu mjini Berlin waliandika barua ya wazi kuthibitisha haki ya wanafunzi kuandamana.
“Bila kujali iwapo tunakubaliana na matakwa maalum ya kambi ya maandamano, tunasimama na wanafunzi wetu na kutetea haki yao ya maandamano ya amani,” waliandika.
Soma pia: Ujerumani yajitetea katika mahakama ya ICJ
Polisi walisema watu 79 walizuiliwa kwa muda kufuatia maandamano hayo mwezi Mei, huku uchunguzi wa visa 80 vya uhalifu na kesi 79 za makosa zikianzishwa.
Katika taarifa yao, wahadhiri hao waliitaka “menejimenti ya chuo kikuu kujiepusha na operesheni za polisi dhidi ya wanafunzi wao wenyewe na vile vile kufunguliwa mashtaka zaidi ya jinai.”
Wakati huo, Stark-Watzinger aliikosoa barua ya wasomi hao kwa kutotaja mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyofanywa na kundi la Hamas na wanamgambo wengine kusini mwa Israel. Alirudia ukosoaji huo siku ya Jumapili. Hamas imeorodheshwa kama shirika la kigaidi na Marekani, Umoja wa Ulayana wengine.