NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, amesema Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa kasi na kwa ufanisi kama kilivyoahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
Hayo ameyasema wakati akizungumza na Mtumishi wa Chama hicho Sheikh Salum Msabaha huko nyumbani kwake Fuoni, Wilaya ya Magharibi ‘’A’’ Unguja.
Alisema wananchi wanahitaji maendeleo endelevu ili wapate unafuu wa maisha katika masuala mbali mbali ya kiuchumi na kijamii.
Dkt.Dimwa, alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kumfariji mtumishi huyo wa Chama Cha Mapinduzi anayeumwa kwa muda mrefu ili awe na matumaini ya kuamini kuwa bado viongozi na watendaji wa Chama wanathamini mchango wake mkubwa wa kiutendaji katika ngazi mbali mbali za Chama.
“Chama Cha Mapinduzi kinathamini sana mchango wako katika utekelezaji wa majukumu na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akuafu na kukujaalia afya njema ili upone na kurudi kazini ili tuendelee kushirikiana katika kuimarisha Chama chetu.”, alisema Dkt.Dimwa.
Alifafanua kuwa Chama kitaendelea kutoa mchango wake katika kusimamia masuala ya matibabu ili kuhakikisha mtumishi huyo anapona ili aendelee na majukumu yake.
Kupitia ziara hiyo Dkt.Dimwa, alisema CCM ni daraja baina ya wananchi na Serikali katika kusimamia masuala mbalimbali ya maendeleo yanayotoa fursa pana ya kunufaika kiuchumi kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Naye Mtumishi huyo Salum Msabaha, amempongeza Naibu Katibu Mkuu Dkt.Dimwa kwa kazi kubwa anayofanya katika kuimarisha Chama Cha Mapinduzi nchini katika nyanja za kisiasa,kiitikadi,kiutendaji na kiungozi.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa (upande wa kulia),akizungumza na Mtumishi wa Chama Cha Mapinduzi Sheikh Salum Msabaha (upande wa kushoto) alipomtembelea kwa ajili ya kumjulia hali yake kutokana na kuumwa kwa muda mrefu huko nyumbani kwake Fuoni Wilaya Magharib ‘B’.